UN: Kuongezewa adhabu ya kifungo Sheikh Salman ni ukandamizaji wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8305-un_kuongezewa_adhabu_ya_kifungo_sheikh_salman_ni_ukandamizaji_wa_kisiasa
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya uhuru wa maoni na uhuru wa kujieleza amelaani vikali uamuzi wa mahakama ya rufaa ya Bahrain wa kuidhinisha hukumu iliyotolewa dhidi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Al-Wifaq na kuongeza adhabu hiyo ya kifungo hadi miaka tisa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 02, 2016 03:18 UTC
  • UN: Kuongezewa adhabu ya kifungo Sheikh Salman ni ukandamizaji wa kisiasa

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya uhuru wa maoni na uhuru wa kujieleza amelaani vikali uamuzi wa mahakama ya rufaa ya Bahrain wa kuidhinisha hukumu iliyotolewa dhidi ya Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Al-Wifaq na kuongeza adhabu hiyo ya kifungo hadi miaka tisa.

David Kaye, ameyasema hayo mjini Geneva, Uswisi na kueleza kwamba uamuzi huo wa viongozi wa Bahrain unaonesha kuwepo kwa "mwenendo unaotia wasiwasi wa ukandamizaji wa kisiasa" nchini humo.

Mtaalamu huyo wa masuala ya haki za binadamu ameongeza kuwa:" inavyoonesha, adhabu ya kifungo aliyopewa Sheikh Salman inathibitisha kuwepo mwenendo wa kutia wasiwasi wa ukandamizaji wa kisiasa nchini Bahrain unaozidi kubana fursa ya kuchukuliwa hatua yoyote ya upinzani nchini humo. Kujichukulia uamuzi wa kutoa hukumu ya kifungo cha miaka tisa jela dhidi ya kiongozi maarufu wa kisiasa kama huyu bila ya shaka kutakuwa na taathira kubwa sana hasi kwa jamii nzima".

Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq, ambayo ndiyo harakati kuu ya upinzani nchini Bahrain alitiwa nguvuni mwezi Desemba mwaka 2014 baada ya kutoa hotuba kadhaa za kupinga siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Mnamo mwezi Juni mwaka jana, utawala wa kidikteta wa ukoo wa Aal Khalifa ulimhukumu Katibu Mkuu huyo wa harakati ya al-Wifaq kifungo cha miaka minne jela kwa tuhuma bandia za kuchochea wananchi ili kuuondoa madarakani utawala huo wa kifalme.

Siku ya Jumatatu mahakama ya rufaa ya nchi hiyo ilitoa hukumu ya kuongeza hadi miaka tisa adhabu ya awali ya kifungo cha miaka minne jela aliyokuwa amepewa Sheikh Salman.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Salman alipelekwa uhamishoni katika muongo wa 1990 na akarejea nchini mwake mwaka 2001.

Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa vuguvugu la mapinduzi ya wananchi wanaopinga utawala wa kifamilia wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanapigania uhuru, uadilifu, kuhatimishwa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe.../