Wanajeshi wa Israel wampiga risasi na kumuua mwanamke Mpalestina
Wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wamempiga risasi na kumuua shahidi mwanamke Mpalestina kwa kisingizio kuwa eti alikuwa analenga kutekeleza shambulizi la kujitolea kufa shahidi.
Mwanamke huyo Mpalestina amepigwa risasi kadhaa na askari hao makatili wa Israel leo Jumatano asubuhi karibu na kambi ya al-Uroub, kaskazini mwa al Khalil, mji ulio katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Hilali Nyekundu ya Palestina imesema wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliwazuia wafanyakazi wa afya kufika katika eneo la jinai hiyo na kuongeza kuwa mwanamke huyo alikimbizwa hospitali kwa kuchelewa sana.
Wizara ya Afya imemtambua mwanamke huyo kuwa ni Ghufran Haroun Hamed Warasneh, aliyekuwa na umri wa miaka 31 na ambaye amewahi kushikiliwa katika jela za kuogofya za Israel.
Jumanne pia walowezi wa Kizayuni walishambulia nyumba za Wapalestina huko Silwan, mashariki mwa mji wa Quds (Jerusalem) na kuwajeruhu vijana watatu Wapalestina.
Mivutano na hali ya wasiwasi imeshtadi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kufuatia hatua ya walowezi wa Kizayuni ya kufanya maandamano katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilitangaza hapo awali kuwa Wapalestina wasiopungua 200 walijeruhiwa katika mashambulio ya siku ya Jumapili yaliyofanywa na Wazayuni katika eneo la mashariki la mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na pia katika Ufukwe wa Magharibi.
Siku ya Jumapili walowezi wengi wa Kizayuni walishiriki katika kile kinachoitwa maandamano ya bendera huku wakilindwa na kusindikizwa na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mitaa na barabara za eneo la kale la mji wa Quds, hatua ambayo imekabiliwa na jibu kali la Wapalestina na watetezi wa mji huo na msikiti wa al Aqsa.