Bunge la Iraq lalaani kuvunjiwa heshima Mtume SAW nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i84500-bunge_la_iraq_lalaani_kuvunjiwa_heshima_mtume_saw_nchini_india
Bunge la Iraq limelaani vikali hatua ya baadhi ya viongozi wa chama tawala nchini India ya kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Jun 07, 2022 23:10 UTC
  • Bunge la Iraq lalaani kuvunjiwa heshima Mtume SAW nchini India

Bunge la Iraq limelaani vikali hatua ya baadhi ya viongozi wa chama tawala nchini India ya kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW.

Taarifa iliyotolewa na moja ya kamisheni za Bunge la Iraq imeitaka serikali ya Baghdad kumuita balozi wa India aliyeko nchini humo na kumkabidhi malalamiko yake kuhusiana na kuvunjiwa heshima Bwana Mtume SAW.

Sehemu nyingine ya taarifa ya kamisheni hiyo imeeleza kuwa, utovu huu wa adabu, hatua za makusudi na za fedheha dhidi ya Mtume SAW zitakuwa na matokeo mabaya na yumkini itakaposhindikana kudhibitiwa matokeo yake yatakuwa mabaya mno.

Kadhalika taarifa hiyo imebainisha kwamba, Uislamu ni dini ya amani na Mtume SAW ni mbebaji wa bendera ya dini hii na ni Mtume wa Allah, hivyo hatua yoyote ya kumvunjia heshima Mtume yeyote yule wa Allah, dini au itikadi ya watu fulani ni jambo linalokemewa na lisilokubalika kwa mujibu wa sheria ziliozowekwa na Umoja wa Mataifa.

Naveen Kumar Jindal na Nupur Sharma ni wanachama wa BJP India waliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

 

Katika mdahalo wa televisheni, msemaji wa chama tawala cha India, BJP, Nupur Sharma alitoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Mtume wa Uislamu, ambayo yamelaaniwa kote India na kuibua ghasia nchini humo. 

chama cha BJP kilitangaza kusimamisha uanachama wa Sharma na kujiweka mbali na matamshi yake yenye chuki.

Aidha chama hicho kimemfukuza kazi Naveen Kumar Jindal ambaye anasimamia kitengo cha habari cha chama hicho mjini New Delhi ambaye pia alituma ujumbe uliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW katika ukurasa wake wa Twitter na kufuatia malalamiko alifuta ujumbe huo.