Aug 27, 2022 03:24 UTC
  • Mashambulizi haramu ya Marekani nchini Syria, nembo ya ubeberu wa Washington

John Kriby, mratibu wa mahusiano ya kiistratijia ya baraza la usalama wa taifa la ikulu ya Marekani, White House amejaribu kuhalalalisha mashambulio haramu ya nchi yake huko Syria na kudai kuwa, eti Washington haina nia ya kuzidisha machafuko katika eneo hili.

Vile vile amedai kuwa, lengo la mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani huko Syria eti yalikuwa ni maghala ya silaha na miundombinu ya kijeshi.

Msemaji mmoja wa kijeshi wa Marekani naye amesema, ndege nane za kivita za nchi hiyo ambazo zilijumuisha ndege nne za F-16 na ndege nne za F-15 zilishambulia maeneo 9 tofauti ya Syria Jumatano asubuhi. Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon naye amedai kuwa, Washington haitosita hata kidogo kulinda maafisa wake. Lakini hapa hapa swali linalojitokeza ni kuwa, Marekani imepeleka maafisa wake kwenda kuikalia kwa mabavu ardhi ya Syria kwa idhini ya nani? Si Umoja wa Mataifa umeipa ruhusu na si serikali ya Damascus imeialika, bali ni ubeberu wake tu ndio ulioifanya Marekani ipeleke wanajeshi wake vamizi huko Syria.

Mashambulio ya hivi karibuni ya Marekani nchini Syria yamelalamikiwa vikali duniani ukiwemo Umoja wa Mataifa. Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelalamikia mashambulizi hayo na kuitaka Marekani iheshimu haki ya kujitawala nchi ya Syria. Amesema, Umoja wa Mataifa una wasiwasi kutokana na mashambulio kama hayo hasa kwa kuzingatia hali tete iliyopo kwenye eneo hili. Pia amezitaka pande hasimu nchini Syria kuvumiliana na zijiepushe na kuhatarisha zaidi hali ya mambo nchini humo.

Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani jinai za Marekani nchini Syria

 

Kiujumla ni kuwa mashambulizi ya kijinai ya Marekani nchini Syria yamekuwepo tangu miaka kadhaa nyuma tangu ulipoundwa muungano eti wa kimataifa wa kukabiliana na magaidi wa Daesh; kundi la ukufurishaji ambalo limeundwa na kupewa mafunzo ya kijeshi na hao hao Wamarekani. Kwa kweli inachofanya Marekani huko Syria ni kuua raia tu na kuiba utajiri wa nchi hiyo ya Kiarabu hasa mafuta. Katika ripoti zake kadhaa, gazeti la New York Times limewanukuu maafisa mbalimbali wa zamani wa kijeshi wa Marekani wakifichua jinai kubwa zinazofanywa na mashambulizi ya Marekani dhidi ya raia wa Syria.

Jinai za moja kwa moja za Marekani dhidi ya wananchi wa Syria zimekuwa zikiendelea kwa zaidi ya muongo mmoja sasa yaani tangu mwaka 2011 kwa kuunda magenge ya kigaidi na kuyamimina nchini Syria ambako yamefanya jinai za kikatili na za kutisha dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali ya Syria na hadi hivi sasa Marekani inaendelea kufanya jinai hizo kwa madai ya kupamba na magenge hayo hayo ya kigaidi iliyoyoyaunda na kuyamimina ndani ya ardhi ya Syria.

Katika jinai kubwa za Marekani vamizi, ni kujaribu kukwangura akiba ya utajiri wa mafuta ya Syria

 

Kama ilivyofanya miaka mingi huko nyuma, serikali ya Marekani hivi sasa pia chini ya urais wa Joe Biden inakanyaga misingi na sheria zote za kimataifa, imeivamia Syria bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa wala mwaliko wa serikali ya Damascus, inaiba utajiri wa mafuta ya nchi hiyo na inaendelea kufanya jinai dhidi ya raia wa Syria kwa madai ya eti kulinda askari wake kana kwamba ina kibali cha kuwa na askari wake nchini humo. Kwa kweli Biden anaendeleza siasa zile zile za kibeberu za Marekani dhidi ya mataifa ya dunia na hasa kambi ya muqawama inayopambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. John Kriby, wakati huo akiwa msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon alisema kijuba na kijeuri mwezi Januari 2021 kwamba Washington haina haja wala idhini ya yeyote katika mashambulio yake ya anga nchini Syria.

Tab'an si Umoja wa Mataifa na Serikali ya Damascus pekee inayolalamikia jinai za Marekani huko Syria bali mataifa yote huru na yenye hisia za utu duniani, yanalaani vikali jinai hizo. Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov alisema, Marekani inafanya njama za kuiba kadiri inavyoweza utajiri wa Syria katika wakati huu ambapo serikali ya Damascus inapambana na magaidi (waliomiminwa huko Syria na madola hayo hayo ya Magharibi). Marekani imeunda serikali ndani ya ardhi ya Syria kinyume kabisa na sheria zote za kimataifa na sasa hivi inachochea baadhi ya makundi kujitenga na ardhi ya Syria.

Tags