UN: Israel imeua makumi ya Wapalestina ndani ya wiki tatu
Vikosi vya utawala haramu wa Israel vimewaua shahidi makumi ya Wapalestina katika kipindi cha wiki tatu, katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu, hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika ripoti yake ya jana Jumamosi iliyopewa anuani ya 'Kuwalinda Raia' kuwa, kwa akali Wapalestina 31 wameuawa, huku makumi ya nyumba zikiteketezwa kwa moto na wanajeshi wa Israel baina ya Januari 10 na 30.
OCHA imeeleza katika ripoti yake hiyo kuwa, miongoni mwa Wapalestina waliouawa shahidi na wanajeshi wa Israel, ni watoto 10 wa Kipalestina waliouawa katika shambulizi la vikosi vya Israel la Januari 26 katika mji wa Jenin.
Shirika la habari la WAFA limenukuu ripoti hiyo ya Ofisi ya UN ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ikisema kuwa, Wapalestina 441 wakiwemo watoto wadogo 49 wamejeruhiwa katika uvamizi na hujuma hiyo ya askari makatili wa Israel ndani ya muda huo.
OCHA imeongeza kuwa, Wapalestina 99 wakiwemo watoto 54 wameachwa bila makazi kutokana na uvamizi huo wa wanajeshi wa Kizayuni, huku wengine 21,000 wakiathiriwa moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na mashambulio hayo.
Kwa mujibu wa takwimu mpya za shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, vikosi vya Israel vimewaua karibu Wapalestina 220 katika miezi ya karibuni, wakiwemo 35 mnamo Januari 2023 pekee.
Limesema utawala wa Israel lazima uvunje mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid ambao unasababisha mateso na umwagaji damu mkubwa" katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.