Syria yakosoa 'upotoshaji' wa Marekani kuhusu kuondoa vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i93942-syria_yakosoa_'upotoshaji'_wa_marekani_kuhusu_kuondoa_vikwazo
Serikali ya Syria imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kutangaza kuisimamishia vikwazo nchi hiyo ya Kiarabu kwa muda wa miezi sita, eti ili kuruhusu kupelekwa misaada ya dharura katika taifa hilo lililokumbwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2023 23:05 UTC
  • Syria yakosoa 'upotoshaji' wa Marekani kuhusu kuondoa vikwazo

Serikali ya Syria imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kutangaza kuisimamishia vikwazo nchi hiyo ya Kiarabu kwa muda wa miezi sita, eti ili kuruhusu kupelekwa misaada ya dharura katika taifa hilo lililokumbwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi hivi karibuni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema katika taarifa kuwa, hatua hiyo ya Marekani ya kudai eti imeliondolea taifa hilo vikwazo kwa muda ni upotoshaji wa wazi na kuihadaa dunia.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kitendo hicho cha kinafiki cha Marekani hakitofautiani na hatua zilizochukuliwa na Washington huko nyuma, na kwamba hali ya halisi inayoshuhudiwa Syria ni tofauti na madai hayo ya upotoshaji ya Marekani.

Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amepuuzilia mbali tangazo hilo la Marekani la eti kuiondolea vikwazo Syria kwa muda wa miezi sita kwa misingi ya ubinadamu.

Sheikh Naim Qassim amesisitiza kuwa, utawala wa Marekani umewawekea wananchi wa Syria vikwazo shadidi vya kikatili kwa miaka mingi sasa, na sasa inajaribu kuipotosha dunia kuwa inajali masuala ya ubinadamu kwa kusimamisha vikwazo hizo kwa muda. 

Marekani imetangaza hatua hiyo ya kinafiki baada ya viongozi wa Syria kusisitiza kuwa, kinachozidisha hali mbaya ya sasa kwa watu waliokumbwa na janga la tetemeko la ardhi ni vikwazo vya Marekani na Ulaya dhidi ya Syria.

Alkhamisi iliyopita, Rais Bashar al-Assad wa Syria alifichua kuwa, Marekani inatoa mashinikizo kwa nchi zinazotaka kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Syria. 

Tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari na hadi sasa limesababisha vifo vya zaidi watu elfu 25 katika nchi hizo mbili.