Wapalestina wengine 3 wauawa shahidi Ukingo wa Magharibi
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameendeleza jinai zao za umwagaji damu kwa kuwaua shahidi Wapalestina watatu katika mji wa Nablus katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Shirika la habari la Ma'an la Palestina limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mauaji hayo ya kikatili yamefanyika alfajiri ya leo Jumapili, baada ya wanajeshi wa Kizayuni kulishambulia kwa risasi gari lililokuwa limewabeba Wapalestina wanne karibu na kambi ya kijeshi ya Sarra, kusini magharibi mwa Nablus.
Nalo shirika la habari la WAFA limesema Wapalestina watatu miongoni mwao wameuawa kigaidi katika hujuma hiyo, na muda mfupi baadaye, askari makatili wa Israel wakavamia maduka yaliyopo karibu na eneo la tukio na kuchukua kwa nguvu kamera za CCTV ili kuficha ukatili huo.
Wanajeshi wa utawala ghasibu unaoikalia Quds Tukufu na Masjidul Aqsa kwa mabavu wameshadidisha hujuma zao katika wiki za hivi karibuni, huku wakiwalenga kwa risasi za moja kwa moja raia wa Palestina wasio na ulinzi.
Jumanne iliyopita wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia mji wa Jenin na kuua Wapalestina wasiopungua 6. Kundi la Muqawama wa Kiislamu la Arin al Usud (Pango la Simba) limesisitiza kuwa litalipiza kisasi cha mauaji ya kikatili ya Wapalestina katika mji huo wa Jenin katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Hujuma hiyo ilifanyika sambamba na mashambulizi mengine ya jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Nablus, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu.
Takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina zinaonesha kuwa, Wapalestina 84 wakiwemo watoto wadogo 15 wameuawa shahidi na jeshi la utawala haramu wa Israel tangu kuanza mwaka huu wa 2023, hasa katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.