Amnesty International: Utawala wa Bahrain ungali unakandamiza uhuru wa kujieleza
(last modified Sat, 01 Apr 2023 09:19:35 GMT )
Apr 01, 2023 09:19 UTC
  • Amnesty International: Utawala wa Bahrain ungali unakandamiza uhuru wa kujieleza

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa, utawala wa kifalme wa Bahrain umeendelea kukandamiza uhuru wa kujieleza na kuendelea kuwashikilia wafungwa raia wanaoukosoa utawala huo.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, Amnesty International imethibitisha kwamba "Bahrain iliendelea katika mwaka uliopita wa 2022, kukandamiza uhuru wa kusema na kukusanyika, na kuwaweka kizuizini wafungwa kwa kutumia haki hizi.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya Amnesty International inaeleza kwamba, "wafungwa waliteswa kikatili na kufanyiwa unyama mkubwa, ikiwa ni pamoja na kupuuzwa na kucheleweshwa kupatiwa matibabu kama njia ya kulipiza kisasi, sambamba kuzuiwa kuwasiliana na familia zao.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, wanaharakati wengi na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Bahrain wameendelea kutoa mwito wa kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain ya kutaka kuachiliiwa huru wafungwa wa kisiasa

 

Utawala wa kiimla nchini Bahrain umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa utawala wa Saudi Arabia kupambana na maandamano na vuguvugu la umma la kupigania mageuzi ya kidemokrasia.

Tangu wakati huo Bahrain imekumbwa na vuguvugu la harakati za mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka kuwa huru, kutekelezwa uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Mbali na adhabu za vifungo, utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia pia mamia ya Wabahrain katika kesi bandia zilizoendeshwa kwa umati na mahakama za utawala huo wa kifalme.