Wataalamu wa UN: Israel iwajibishwe kwa mauaji ya Khader Adnan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i96988-wataalamu_wa_un_israel_iwajibishwe_kwa_mauaji_ya_khader_adnan
Wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa wametaka Israel iwajibike kwa mauaji ya Khader Adnan, kiongozi Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ambaye alikata roho na kufa shahidi akiwa anashikiliwa katika jela ya Israel kufuatia mgomo wa kususia kula kwa muda wa siku 87.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2023 04:47 UTC
  • Wataalamu wa UN: Israel iwajibishwe kwa mauaji ya Khader Adnan

Wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa wametaka Israel iwajibike kwa mauaji ya Khader Adnan, kiongozi Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina ambaye alikata roho na kufa shahidi akiwa anashikiliwa katika jela ya Israel kufuatia mgomo wa kususia kula kwa muda wa siku 87.

Francesca Albanese, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, na Tlaleng Mofokeng, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki ya afya, wametoa wito huo huku wakikemea vikali kile walichokiita kuwaweka kizuizini Wapalestina kwa halaiki kwa sura na hali ya "ukatili" na "unyama" kunakofanywa na Israel.

"Lazima kuwe na uwajibikaji kwa mauaji ya Mpalestina Khader Adnan mwenye umri wa miaka 45 aliyefariki kwa kususia kula" wameeleza wataalamu hao wa UN.

Albanese na Mofokeng wamesisitiza kuwa, kifo cha Khader Adnan ni ushuhuda wa kutisha wa sera na vitendo vya ukatili na vya kinyama vya uwekaji watu kizuizini vinavyofanywa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, pamoja na kushindwa Jamii ya Kimataifa kuuwajibisha utawala huo dhalimu kwa ukiukaji wa sheria unaofanya dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza zaidi kuwa, ni jambo la udharura zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote kwa Jamii ya Kimataifa kuiwajibisha Israel kwa vitendo vyake haramu katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu na kukomesha uhalalishaji wa jinai za kivita inazofanya, ambazo zimekuwa ndio hali halisi ya kila siku katika maisha ya Wapalestina.

Shahidi Khader Adnan alitiwa nguvuni na kuwekwa kizuizini mnamo Februari 5 na kuanzia hapo akasusia kula kulalamikia kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.

Wanamuqawama wa Palestina

Adnan alikuwa akikabiliwa na matatizo makubwa ya kiafya kutokana na mgomo huo, ikiwa ni pamoja na kutapika damu mara kwa mara, kuishiwa nguvu sana, kupoteza fahamu mara kwa mara na kushindwa kuongea, kutembea na kulala kutokana na maumivu makali aliyokuwa nayo mwili mzima.

Kwa muda wa miongo miwili iliyopita, Shahidi Khader Adnan aliwahi kukamatwa mara kadhaa na vikosi vya utawala katili wa Israel kutokana na harakati zake za kisiasa na kupinga uvamizi na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na alipitisha kipindi cha miaka minane kwenye magereza ya utawala huo wa Kizayuni.

Wakati huohuo makundi ya muqawama wa Palestina yameapa kuwa yatalipiza kisasi cha damu ya Sheikh Khader Adnan aliyefia shahidi ndani ya jela ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa za makundi hayo zimesisitiza kuwa, utawala haramu wa Kizayuni ndio unaobeba dhima kamili ya jinai hiyo na utalipa gharama ya unyama huo uliotenda.../