UN yatahadharisha kuhusu mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina
-
Volker Türk
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hali ya isiyodhibitiwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo kadhaa ya Wapalestina.
Katika taarifa yake iliyotolewa kufuatia mashambulizi hayo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN amewataka viongozi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel kuheshimu sheria za kimataifa kuhusu utumiaji nguvu za mauaji.
Volker Türk ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina wa mauaji yanayofanywa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kuwepo ushahidi wa kutosha wa ukiukwaji wa sheria za kitaifa na kimataifa, na kuwajibishwa wanaofanya mauaji hayo.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamuu wa Umoja wa Mataifa amesema, Israel inalazimika kupitia upya sera na taratibu zake katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi na kuheshimu haki ya kuishi ya watu wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, kama dola vamizi. Vilevile inapaswa kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu, na kutekeleza majukumu ya kuhakikisha utulivu na usalama wa umma katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Mashambulizi yaliyoanzihwa na jeshi la Israel dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Jenin mnamo Juni 19 yamepelekea kuuawa shahidi Wapalestina saba wakiwemo watoto wawili na wengine 91 kujeruhiwa.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Israel pia imeua Wapalestina wasiopungua 179 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, wakiwemo watoto 30.
Kwa msingi huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, ili kukomesha mfululizo huu wa ghasia, uvamizi na mashambulizi hayo lazima yakomeshwe katika sura zake zote.