Aug 06, 2023 02:29 UTC
  • Rais wa Venezuela: White House ilipanga njama niuawe

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amemtuhumu aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump kwamba alikuwa mstari wa mbele katika kupanga njama iliyofeli ya kuuawa kiongozi huyo wa Amerika ya Latini.

Maduro amefichua hayo katika hotuba yake mbele ya Kongamano la Kuadhimisha Miaka 86 tangu kuasisiwa Gadi ya Taifa ya nchi hiyo, ambayo imesadifiana na siku iliyofeli njama hiyo ya kuuawa kwake miaka 5 iliyopita.

Amesema Trump mnamo mwaka 2018 aliiagiza White House ya Marekani impange mkakati ya kuuawa rais huyo wa Venezuela kwa shambulizi la ndege isiyo na rubani (droni).

Maduro amebainisha kuwa, Ikulu ya White House ya Marekani ilitaka shambulio hilo lifanywe na kundi moja la kigaidi lenye makao yake katika nchi jirani na Venezuela. 

Aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump

Rais wa Venezuela ameeleza kuwa, uchunguzi wao umebaini kuwa Marekani ilitaka kumtumia rais wa wakati huo wa Colombia, Juan Manuel Santos, kufanikisha njama hiyo iliyotibuka.

Amesema Santos ndiye aliyekuwa mkuu wa mikakati katika njama hiyo iliyoratibiwa na White House, siku chache kabla ya rais huyo wa Colombia kumaliza hatamu zake za uongozi.

Askari kadhaa walijeruhiwa katika shambulio hilo la droni la Agosti 4 mwaka 2018, wakati ambapo Maduro alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara mjini Caracas.

 

 

Tags