Ushuhuda kwa Al Jazeera: Sweden imekuwa nchi ya chuki na ubaguzi dhidi ya wageni na Waislamu
Sweden ambayo imekuwa ikijulikana kama mfano wa ustahamilivu tangu miaka ya 1970, imebadilika sana katika miongo michache iliyopita na kuwa nchi ya ubaguzi wa rangi, kuongezeka kwa vitendo vya chuki dhidi ya wageni na wahamiaji, na kushamiri harakati zenye misimamo mikali za mrengo wa kulia.
Kipindi kilichorushwa hewani jana tarehe 4 Septemba na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kimefichua ushuhuda wa aina yake unaoonyesha kwamba, wahamiaji Waislamu na Waafrika wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kibaguzi vilivyopangwa na maafisa wa polisi na kuwabaguliwa watu hao wazi wazi kwa maslahi ya wazungu.
Ripoti ya al Jazeera inasema: Idadi kubwa ya wahamiaji wanaogopa kuonekana kwenye vyombo vya habari na kuzungumzia mateso na dhulma wanayokabiliana nayo nchini Sweden kwa hofu ya kulipizwa kisasi kutoka kwa harakati za kibaguzi zinazohubiri kuwa watu wenye rangi nyeupe (wazungu) ni bora zaidi kuliko wanaadamu wengine.
Haya yanajiri wakati Umoja wa Mataifa umesema kuwa, Stockholm inalazimika kuongeze juhudi za kukabiliana na ubaguzi wa kimfumo na kujikita kwenye mikakati ya kurejesha uaminifu kati ya polisi na jamii za walio wachache nchini humo.
Ripoti ya uchunguzi wa al Jazeera iliyopewa anwani: "Kisa Kinaendelea", inafichua kuwa, wahamiaji wanaishi kwenye vitongoji vya nje ya miji ya Sweden na wamejirundika katika maeneo yaliyotengwa na yasiyovutia, sambamba na kuteseka kwa ubaguzi wa rangi unaotokana na mwonekano wa rangi ya ngozi zao.
Imesema seikali ya Stockholm inapuuza malalamiko yao ya mara kwa mara, na polisi hawatekeleza jukumu waliyopewa ya kuchunguza uhalifu wa mauaji yanayofanywa dhidi ya wahajiri na jamii za waliowachache na kuwawajibisha wahusika.
Itakumbukwa kuwa, katika miezi ya hivi karibuni, watu wenye misimamo mikali wamekuwa wakihujumu matukufu ya Waislamu nchini Sweden ikiwa ni pamoja kuchoma moto Qur'ani Tukufu katika maeneo ya umma na mbele ya misikiti kwa usimamizi na himaya ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo.