Sep 25, 2023 13:26 UTC
  •  Yván Gil
    Yván Gil

Nafasi ya dola kama sarafu inayotumika zaidi katika uwekezaji na miamala ya malipo katika biashara na uchumi wa dunia tokea mwanzoni mwa karne hii imepa Marekani fursa kuitumia sarafu hiyo kama wenzo wa kuziwekea nchi nyinginezo vikwazo vya kifedha na kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripori ya Shirika la Habari la Iran (IRNA), Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yván Gil, amesema kuwa hivi karibuni tushuhudia mbadala wa sarafu ya dola katika biashara ya dunia na sarafu ya dola itapoteza thamani yake katika siku za usoni.

Gil ameongeza kuwa, kuanzishwa mfumo mpya duniani  kutasaidia kuleta uwino katika kuhakikisha kuwa dola sio chaguo pekee linalotumika katika miamala ya kibiashara.

Akiashiria mwenendo unaokua wa miamala ya biashara ya nishati kwa kutumia sarafu nyingine zisizokuwa dola ya Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema kuwa, nchi zenye uwezo ya chakula za Latin Amerika kama vile Brazili na Argentina, zinaendeleza miamala yao ya kibiashara kwa kutumia sarafu zinginezo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesisitiza kuwa hivi sasa dola ya Marekani inatumika kama silaha ya mabavu dhidi ya nchi nyingine, na kuongeza kwamba, kuibuka sarafu nyingine kutaleta utulivu katika mabadilishano ya kibiashara ulimwenguni.

Mwenendo wa kufutilia mbali safaru ya dola duniani ulishika kasi baada ya serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani kuanza kuiwekea Russia vikwazo kwa kisingizio cha vita vya Ukraine, na sasa idadi kubwa ya nchi zimeanza kutafuta njia mbadala ya kuondoa safaru hiyo katika miamala ya biashara za kimataifa na mabadilishano ya kiuchumi.