Mwakilishi wa Uhispania katika Bunge la Ulaya: Israel imekufa
Mwakilishi wa Uhispania katika Bunge la Ulaya amesema, "Israel" imekufa, na licha ya kuuawa shahidi maelfu ya watu huko Gaza, Wapalestina wanakaribia zaidi kupata ushindi.
Manuel Pineda, amesema: "Inatosha kutazama uso wa mtoto wa Kipalestina na tabasamu lake, kujua kwamba watu hawa hawawezi kushindwa."
Ameongeza kuwa hii leo walimwengu wanajua kuwa "Israel ni genge la kigaidi" na kampeni inayosema Wayahudi ni wahanga au wana haki ya kuishi Palestina haina tija tena.
Pineda, ambaye alizua mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari katika wiki ya pili ya vita vya Gaza kutokana na kuvaa nembo ya Wapalestina na kuiunga mkono Palestina katika mkutano wa Umoja wa Ulaya ambako alifananisha jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na adhabu ya umati iliyokuwa ikitolewa na Wanazi katika Gheto za Warsaw, siku ya Ijumaa iliyopita pia ilionya juu ya upotoshaji wa ukweli unaofanyika katika vyombo vya habari kuhusu Palestina.
Akihutubia mkutano uliofanyika katika Taasisi ya Urafiki na Watu wa Cuba (ICAP) huko Havana, Manuel Pineda alisema kuwa Wazayuni wanakusudia kuifanya Oktoba 7 na mwanzo wa operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa kuwa ndio chanzo cha kila kitu na kufumbia macho mizizi na chanzo halisi cha mgogoro wa Palestina ambacho ni uvamizi wa Israel.
Mwakilishi wa Uhispania katika Bunge la Ulaya amesema kuwa, hii leo utawala haramu wa Israel hauwezi kuwapigisha magoti watu wa Palestina.
Manuel Pineda amesisitiza kuwa licha ya kuuawa shahidi maelfu ya Wapalestina na kuharibiwa eneo la Ukanda wa Gaza, ushindi uko karibu zaidi ya Wapalestina kuliko wakati mwingine wowote baada ya operesheni ya tarehe 7 Oktoba.