Wanazuoni wa Kiislamu kutuma ujumbe Gaza
Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) umeunda ujumbe ambao utautuma katika Ukanda wa wa Gaza kupitia Misri; huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendelea kuwashambulia kikatili Wapalestina wa eneo hilo lililozingirwa.
Ali Muhyiddin al-Qaradaghi, Katibu Mkuu wa IUMS amesema katika taarifa kuwa, ujumbe wa jumuiya hiyo ya wasomi wa Kiislamu yenye makao yake nchini Doha utaingia Gaza kupitia Kivuko cha Rafah.
Amesema muungano huo umeiomba serikali ya Cairo pamoja na Sheikh Ahmed at-Tayeb, Imam na Kiongozi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar cha nchini Misri kufanikisha mchakato wa safari hiyo.
Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Al-Qaradaghi akisema aliwasilisha ombi Misri la kutaka ujumbe wa taasisi hiyo ya wanazuoni wa Kiislamu usafiri kwenda Gaza kupitia Kivuko cha Rafah mwezi mmoja uliopita, na kwamba binafsi ana hamu ya kuwa wa kwanza kusajiliwa kwenye orodha ya ujumbe huo.

Ujumbe huo wa wanazuoni wa Kiislamu duniani unatazamiwa kuelekea Gaza huku walimwengu wakiendelea kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa wananchi madhulumu wa Palestina kupitia maandamano ya kulaani jinai za Wazayuni.
Huku hayo yakijiri, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulio ya kinyama ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita hadi sasa imepindukia 24,000 na idadi ya majeruhi ni zaidi ya 60,500.