Feb 19, 2024 07:05 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Februari 19

Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri katika kona mbalimbali za dunia ndani ya siku saba zilizopita…

Soka ya Ufukweni

Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Iran imeendelea kung'ara katika fainali za Kombe la Dunia la FIFA, ambapo Jumamosi iliichabanga Argentina mabao 6-3 na kutinga hatua ya mchujo. Mabao ya Mohammad Mokhtari, Hamid Behzadpour na Reza Amiri katika kipindi cha kwanza yaliiweka Iran kifua mbele. Argentina ilipambana kufa kupona na ikafanikiwa kucheza na nyavu mara tatu, lakini mabao mengine ya Mohammad Moradi, Movahed Mohammadpour na Ali Mirshekari yalitosha kufungisha virago timu hiyo ya Amerika ya Latini.

Iran ilitwaa ubingwa wa Asia 2019

 

Mapema Jumamosi, Tahiti iliizaba Uhispania mabao 5-3. Iran ambayo awali iliitandika Uhispania mabao 3-1 katika upigaji matatu baada ya kutoa sare ya mabao 3-3, na ambayo ilimaliza ya tatu katika mashindano ya mwaka 2017, Jumatatu ilivaana na Tahiti na kutuama kileleni mwa Kundi B.

 Ligi ya Mabingwa Asia

Klabu ya soka ya Sepahan ya Iran Alkhamisi usiku iliadhibiwa mabao 3-1 na al-Hilal ya Saudi Arabia katika mchuano wa Ligi ya Mabingwa ya Asia. Bao la dakika ya 37 la Ramin Rezaian liliiweka Sepahan kifua mbele, lakini kwa dakika chache tu. Salamu za msiba zilianza kutumwa kwa Sepahan baada ya al-Hilal kufungua mlango wa mabao kunako dakika ya 57.

Masaibu ya Sepahan yalizidi baada ya Mohammad Daneshgar kutandikwa kadi nyekudu kunako dakika ya 76, na kilochofuata ni majanga.

Riadha ya Walemavu Dubai

Iran imezoa jumla ya medali saba kwenye mashindano ya kimataifa ya wanariadha walemavu huko Dubai, Imarati. Mashindano hayo ya Dubai 2024 Grand Prix – Fazza International Athletics Championships yalifunga pazia lake Ijumaa kwa wanariadha wa Kiirani kuzoa medali 2 za dhahabu, 3 za fedha na 2 za shaba.

Wanariadha 573 kutoka mataifa 71 wameshiriki duru ya 15 ya mashindano ya Grand Prix kusaka tiketi za kushiriki mashindano ya Kobe 2024 World Para Athletics Championships na Michezo ya Paralimpiki ya Paris nchini Ufaransa mwaka huu 2024.

Iran mwenyeji ya mashindano ya riadha Asia

Wanariadha wa Iran wamezoa medali lukuki kwenye mashindano ya riadha ya Asia yaliyofanyika hapa jijini Tehran.  Sajad Aghaei siku ya Jumapili aliipa Iran medali nyingine ya dhahabu baada ya kuibuka kidedea kwenye mbio za mita 400 kwenye duru ya 11 ya mashindano hayo yanayofahamika kama Asian Indoor Athletic Championships.

 

Dhahabu nyingine ya Iran ilitwaliwa na Farzaneh Fasihi katika mbio za mita 60 kwa upande wa akina dada. Siku ya Jumamosi, Mehdi Saberi na Ali Amirian walishinda medali za fedha katika mbio za mita 1500 na urushaji kitufe kwa usanjari huo. Waziri wa Michezo wa Iran, Kiumars Hashemi amesema Jamhuri ya Kiislamu imezimia kuwa kituo cha riadha barani Asia. Hashemi amesema hayo katika mazungumzo na Dahlan Jumaan Al Hamad, Rais wa Shirikisho la Riadha la Asia hapa mjini Tehran. Waziri huyo amelishukuru shirikisho hilo kwa kuichagua Iran kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ya riadha barani Asia yaliyofanyika baina ya Februari 17 na 19. Al Hamad kwa upande wake amesema Iran ni taifa muhimu na lenye ushawishi kieneo na kimataifa, na lina nafasi muhimu katika michezo mbali mbali.

Dondoo za Hapa na Pale

Klabu ya Liverpool imeendelea kutuama kileleni mwa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza (EPL) na kujiweka pazuri kutawazwa mabingwa wa kipute hicho msimu huu baada ya kuitandika Brentford wikendi mabao 4-1 katika Uwanja wa Brentford Community. Darwin Nunez aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao kunako dakika ya 35 kabla ya magoli mengine kufumwa wavuni katika kipindi cha pili kupitia kwa Alexis Mac Allister, Mohamed Salah na Cody Gakpo. Bao la Salah lilikuwa lake la kwanza mwaka huu akivalia jezi za Liverpool. Nyota huyo raia wa Misri alikuwa akiwajibikia Liverpool kwa mara ya kwanza tangu apate jeraha la paja mwezi uliopita akicheza dhidi ya Ghana kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool sasa wanajivunia alama 57 kutokana na mechi 25, na pengo la pointi 2 kati yao na nambari 2 Arsenal walioinyoa kwa chupa Burnley kwa kuigaraza mabao 5-0. Mabao ya Wabeba Bunduki katika mchuano huo wa Jumamosi ugenini yalitiwa nyavuvi na Martin Odegaard, Bukayo Saka (2), Leandro Trossard na Kai Harvetz.

Kylian Mbappe

 

Huku hayo yakijiri, kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amesema Gunners ni lazima iwe kwenye mjadala linapokuja suala la kusajili mchezaji nyota wa kiwango cha Kylian Mbappe. Mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain kwa muda mrefu amekuwa akizungumzwa kutaka kuachana na miamba hiyo ya Ufaransa, na hilo linaweza kutimia mwishoni mwa msimu huu. Hata hivyo, bado hakuna uhakika ni wapi Mbappe hasa atakwenda mwishoni mwa msimu huu baada ya sasa kudaiwa atakwenda Real Madrid.

Wakati huohuo, klabu ya PSG inatafakari kuwasilisha ombi la uhamisho wa kiungo wa FC Barcelona, Pablo Martín Páez maarufu Gavi majira ya kiangazi. PSG kwa muda mrefu wamekuwa wakivutiwa na kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 ambaye jarida la The Athletic la nchini Uhispania limemtaja kwenye orodha fupi ya wachezaji wanaolengwa kwenye dirisha la usajili la msimu wa joto kali. Ikiwa utakamilika uhamisho huo utamfanya Gavi kuungana tena na kocha wake wa zamani Luis Enrique, ambaye alicheza kwa mara ya kwanza walikutana katika klabu ya Barca akiwa na umri wa miaka 17.

Barcelona hawana nia ya kumuuza kiungo huyo kutoka katika academy yao ya La Masia lakini kutokana na hali mbaya ya kifedha, klabu hiyo inaweza kulazimika kumwachia endapo watapata ofa nzuri. Nikukurejesha tena kwenye EPL mpenzi msikilizaji, Manchester City kwa ssa wanaonekana kurdhika na nafasi ya tatu wakiwa na alama 53, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Chelsea.

 

Watani wao wa jadi, Manchester United pia walipata mnyonge na kumzaba mabao 2-1 ugenini. Mabao ya Mashetani Wekundu kwenye mechi hiyo dhidi ya Luton Town yalifungwa na Rasmus Hojlund huku la kufutia machozi la wenyeji likifungwa na Carlton Morris.

Devils kwa sasa wametulia kwenye nafasi ya 6 wakiwa na pointi 44, wakiibeba Tottenham yenye alama 47. Villa wanashikilia nafasi ya 4 wakiwa na alama 49.

…………………MWISHO….………..

 

 

 

 

 

Tags