Guterres: Nimefunga Swaumu ya Ramadhani kuheshimu imani ya Waislamu wa Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amefichua kwamba alifunga Swaumu ya Ramadhani wakati wa safari yake ya mshikamano na watu wa Gaza ili kuonyesha heshima kwa imani za Waislamu aliowatembelea, akimaanisha ziara yake ya kutembelea kivuko cha Rafah siku ya Jumamosi na ziara yake mjini Cairo Jumapili wiki hii.
Guterres amesema hayo katika ujumbe alioandika kwenye akaunti yake jukwaa la X, ambapo pia amesema kwamba alihisi maumivu kwa sababu "Wapalestina wengi huko Gaza hawawezi kula kchakula kinachofaa cha futari"
"Kufunga kwangu wakati wa misheni ya mshikamano wa Ramadhani, ni kwa ajili ya kuheshimu imani ya Waislamu ninaowatembelea. Hata hivyo moyo wangu umevunjika nikijua kwamba Wapalestina wengi huko Gaza hawataweza kupata na Iftar inayofaa", amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake mtandao wa X.
Wakati wa ziara yake katika kivuko cha Rafah kilichoko kwenye mpaka wa Misri na Ukanda wa Gaza, Antonio Guterres alisema: Inasikitisha kuona kwamba malori yenye misaada ya kibinadamu yameegeshwa upande mmoja wa kivuko huku baa la njaa ikitesa watu katika upande wa pili.
Guterres alionya juu ya athari za kimataifa za vita huko Gaza, na kusema kwamba kuna janga la binadamu katika ukanda huo, na kwamba mashambulizi ya kila siku dhidi ya utu wa Wapalestina yanazua mgogoro wa kuaminika kwa jamii ya kimataifa.