Apr 24, 2024 08:09 UTC
  • Watu 5 wafariki dunia wakivuka English Channel, saa chache baada ya kuidhinishwa muswada wa Sunak

Watu wasiopungua 5 wamekufa walipokuwa wakivuka njia ya majini ya English Channel, saa chache baada ya Uingereza kuidhinisha muswada wa kuwafukuza wahamiaji nchini humo na kuwapeleka Rwanda.

Gazeti la Voix du Nord limeripoti kuwa, miili hiyo iligunduliwa katika ufuo wa Wimereaux kaskazini mwa Ufaransa siku ya Jumanne ya jana. Shughuli ya uokoaji inaendelea na helikopta na boti zimetumwa katika eneo hilo.

Takriban wahamiaji 100 wameokolewa na kuwekwa ndani ya meli ya jeshi la wanamaji la Ufaransa. Wahamiaji hao walipangwa kupelekwa kwenye bandari ya Boulogne.

Haya yanajiri saa chache baada ya mpango wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, wa kuwapeleka baadhi ya wahamiaji walioko nchini huko huko Rwanda, kuidhinishwa na Bunge. Mashirika ya kutetea haki za binadamuu yamelaani hatua hiyo na kusema inakiukka haki za haki za binadamu. 

Tume ya Kutetea Haki za Binadamu ya Ulaya, imetoa wito kwa Uingereza kutupilia mbali mpango huo wenye utata wa kuwatuma waomba hifadhi nchini Rwanda.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa Baraza la Ulaya, Michael O'Flaherty, mpango huo wa serikali ya Kigali na Uingereza, unaibua maswali mengi kuhusu haki za waomba hifadhi na sheria kwa ujumla.

Mahakama ya Juu ya Uingereza ilisema mwaka uliopita kwamba, mpango wa serikali ya London wa kuwapeleka nchini Rwanda wakimbizi na waomba hifadhi walioko nchini humo unakiuka sheria. Ilisema mpango huo unawaweka katika hali hatarishi wakimbizi hao, hasa kwa kuzingatia kuwa baadhi yao waliikimbia nchi yao ya Rwanda, na kuwarejesha huko ni kutawaweka hatarini.