Apr 26, 2024 03:07 UTC
  • Mamlaka za uchaguzi India zataka kupewa majibu kuhusu malalamiko dhidi ya Modi na Rahul Gandhi

Mamlaka za uchaguzi India jana zilisema kuwa kuwa zinataka kupewa majibu kutoka chama tawala nchi hiyo cha Bharatiya Janata Party (BJP) na chama kikuu cha upinzani cha Indian National Congress juu ya madai ya ukiukaji wa sheria za uchaguzi katika hotuba zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi zinazoendelea kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo.

Wakati chama tawala cha India cha BJP kikipewa notisi kuhusu hotuba iliyotolewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Narendra Modi wiki iliyopita katika jimbo la Rajasthan magharibi; chama cha upinzani cha  Kongresi  ya Taifa ya India pia kimepewa notisi kufuatia  hotuba iliyotolewa na kiongozi wa chama hicho, Rahul Gandhi. 

Zoezi la kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua wabunge 543 wa bunge la chini la bunge la India  linalojulikana kama Lok Sabha linafanyika kwa awamu saba kuanzia Aprili 19 hadi Juni 1 mwaka huu. Awamu ya pili ya upigaji kura inafanyika leo Ijumaa; ambapo kura zitahesabiwa tarehe Mosi mwezi Juni.

Tume ya Uchaguzi ya India imeeleza katika notisi iliyotolewa kwa Mwenyekiti wa chama tawala cha BJP, Jagat Prakash Nadda kwamba imepokea taarifa kutoka kwa vyama kadhaa vinavyodai kujiri ukiukaji wa sheria za upigaji kura kupitia hotuba zilizotolewa wakati wa kampeni. 

Walalamikaji walilenga zaidi hotuba iliyotolewa na Narendra Modi Waziri Mkuu wa India  ambaye aliwataja Waislamu na wale wenye watoto wengi kuwa ni mamuki wa nyuma ya pazia.

Modi alisema wiki iliyopita katika hotuba yake kuwa na hapa ninamnukuu;"  Hapo awali, wakati wao (chama cha Kongresi akimaanisha chama cha upinzani) walipokuwa madarakani walisema kuwa Waislamu wana haki ya kwanza ya kunufaika na utajiri wa nchi. "Hii ina maana kwamba chama hicho cha upinzani kitagawa utajiri wa nchi, kati ya wale ambao wana watoto wengi  na miongoni mwa mamluki walio nyuma ya pazia akimaanisha Waislamu." 

Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi 

Matamshi hayo yaliyotolewa huko  Rajasthan wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi yalalamikiwa na kukosolewa  na vyama vya upinzani na makundi ya Waislamu na hata chama tawala baadaye kilidai kuwa maoni ya Modi "yalitafsiriwa vibaya."