Ulimwengu wa Spoti, Juni 24
Natumai u bukheri wa afya msikilizaji mpendwa, na karibu tuangazie japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbalimbali za dunia.
Kombe la Dunia; Iran bingwa Zurkhane
Iran ndio mabingwa wa mashindano ya kwanza ya Kombe la Dunia kwenye mchezo wa zurkhaneh, yaliyofanyika katika mkoa wa kati wa Iran wa Isfahan. Duru hiyo ya kwanza ya Kombe la Dunia ya Zurkhaneh imefanyika baina ya Juni 20 na 21, kwa kushirikisha wanamichezo 130 kutoka Tajikistan, India, Syria, Lithuania, Sri Lanka, Iraq, Belarus, Lebanon, Afghanistan, Tanzania, Palestina, Jamhuri ya Azerbaijan, Indonesia, Poland, Pakistan, Burundi, Uzbekistan, Nepal, Estonia, Rwanda na Kenya. Timu ya taifa ya Iran ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuzoa jumla ya pointi 257, huku Jamhuri ya Azerbaijan ikishika nafasi ya pili kwa pointi 185. Ikiwa na alama 170, Iraq ilishika nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo ya kimataifa.

Zurkhaneh, inayomaanisha ‘jumba la nguvu’ kwa lugha ya Kiajemi, ni mahali maalum pa jadi ambapo wanaume hufanya michezo ya kishujaa. Kwa Wairani, mchezo huo unahusishwa na fadhila na wema, na pia ni nembo ya utambulisho wao wa kitaifa.
Sepan yabeba Kombe la Hazfi
Klabu ya Sepahan imetwaa ubingwa wa Kombe la Hazfi (Taji la Muondoano) kwa msimu huu wa mwaka 2023/24. Timu hiyo iliibuka kidedea Alkhamisi baada ya kuigaragaza Mes Rafsanjan mabao 2-0 katika mchezo wa kufa kupona uliopigwa katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran. Mabao mawili yaliyofungwa na nyota wa mchuano huo, Shahriar Moghanlou katika kipindi cha kwanza yalitosha kuifanya Sepahan ibeba kombe hilo kwa mara ya tano sasa. Esteqlal na Persepolis ndizo timu zilizotwa Kombe la Hazfi mara nyingi zaidi; kwani zimelibeba mara 7 kila moja. Michuano ya Hazfi huandaliwa kila mwaka na Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Na timu ya mieleka mtindo wa Greco-Roman ya Iran imeibuka mshindi wa pili wa Mashindano ya Ubingwa ya Asia kwa Vijana wenye chini ya miaka 17. Iran imemaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo yaliyofanyika Amman, mji mkuu wa Jordan baada ya kuzoa medali 3 za dhahabu, 4 za fedha na 3 za shaba na kukusanya jumla ya alama 200. Uzbekistan imeibuka kidedea huku Kazakhstan ikimaliza mshindi wa tatu.
Maafande mabingwa Ligi Kuu ya Soka Zanzibar
Klabu ya JKU imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa mwaka 2023/2024 licha ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kipanga katika mechi ya kufunga pazia la ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan visiwani humo. JKU na Zimamoto ndizo zilizokuwa zikiwania ubingwa huo uliokuwa wazi baada ya wakishikilizi wa taji hilo, KMKM kulitema mapema. Aidha siku ya Jumapili, Maafande wa JKU walinusurika kula kichapo katika mchuano wa funga kazi, waliposhuka dimbani kuvaana na Muembe Makumbi. Walitoshana nguvu na kutoa sare ya mabao 2-2. Kwa matokeo hayo, JKU imefikisha pointi 67 na kukaa kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ambayo ilishirikisha timu 16 kutoka Pemba na Unguja.

Nafasi ya pili katika ligi hiyo ilichukuliwa na Zimamoto yenye pointi 62 huku KMKM yenye pointi 57 ikimaliza ya tatu na KVZ ilikamilisha 'Top Four' ikiwa na pointi 56. JKU sasa itaiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, huku Chipukizi ya Pemba, ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), wakikata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Wakati huo huo, Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamesema malengo yao kuelekea msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2024/2025 ni kufika hatua ya nusu fainali, fainali au kubeba taji la Afrika. Msimu uliopita, Yanga ilitolewa katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema jeuri ya kuzungumza matarajio hayo wanaipata kutokana na kikosi kilichopo, na kile ambacho watakiongeza kuelekea msimu ujao.
Na Kocha Luis de la Fuente amemiminia sifa vijana wake wa Uhispania baada ya kuwafanya mabingwa watetezi Italia waonekana vibonde kwa kuwatandika bao 1-0 na kutinga 16-bora kwenye Kombe la Ulaya (Euro) siku ya Alhamisi. Mabingwa wa UEFA Euro 1964, 2008 na 2012, Uhispania walizamisha Wataliano kupitia bao la kujifunga kutoka kwa beki Riccardo Calafiori dakika ya 55. Ulikuwa ushindi mtamu kwenye ngoma hiyo ya Kundi B dhidi ya Italia ambao hawakuwa wamepoteza michuano 10 mfululizo kwenye mechi za Euro.

Siku hiyo pia, miamba ya soka Ulaya, Denmark na Uingereza zilikuwa zikikabana koo na mechi yao ikaishia kwa sare ya 1-1. Katika matokeo ya mechi nyinginezo, Slovenia ilaimbulia sare ya 1-1 Serbia katika mchuano wa Kundi C, huku Denmark wakiilazimisha Uingereza pia sare ya bao 1-1 kwenye mechi nyingine ya kundi hilo. Uturuki ililishwa kichapo cha mbwa cha mabao 3-0 na Ureno wikendi katika mchuano wa Kundi F. Mechi nyingine iliyovutia ni ile ya Kundi E, ambapo Ubelgiji iliikandamiza Romania mabao 2-0. Mchuano wa Kundi A kati ya Uswisi vs Ujerumani uliopigwa wikendi uliishia kwa sare ya bao 1-1, wakati ambapo Scotland ilikuwa inazabwa bao 1-0 na Hungary.
……………………TAMATI………………