Watu tisa wauawa katika shambulio mjini Munich, Ujerumani
Watu tisa wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kuwafyatulia risasi watu katika jumba moja la kibiashara mjini Munich, Ujerumani.
Operesheni kubwa ya kiusalama inaendelea katika jumba la kibiashara la Olympia, ambalo linapatikana mtaa wa Moosach, kaskazini magharibi mwa mji wa Munich. Watu walioshuhudia tukio wanasema kuwa, wamewaona watu watatu waliokuwa na bunduki.
Polisi wanasema washukiwa bado hawajakamatwa na wamewatahadharisha watu na kuwashauri kutotoka nje.
Wanachunguza iwapo mmoja wa waliofariki ni mtuhumiwa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa watu watatu wanashukiwa kushiriki tukio hilo, ambao waliwakabili polisi kwa majibizano ya risasi na mmoja anadaiwa kuuawa.
Msemaji wa Polisi, Claudia Kuntzel amesema watuhumiwa wamefunga lango linalotizamana na uwanja wa 1972 Olympia na kwamba, kufuatia tukio hilo hali ya hatari imetangazwa na wakazi wa mji huo wamewekewa amri ya kutotembea ovyo, kufungwa kwa biashara na usafiri wa umma.
Watu wengi wamekwama kutokana na kusitishwa kwa usafiri hali ambayo imesababisha adha na usumbufu mkubwa.
Maafisa wa polisi wamekuwa katika hali ya tahadhari tangu Jumatatu baada ya kijana mhamiaji kuwadunga visu na kuwajeruhi watu kadhaa katika treni, na kundi la kigaidi la Daesh kutangaza kwamba, aliyetekeleza shambulio hilo ni mwanachama wake.