Marekani yapinga tena rasimu ya azimio la kusitisha vita, Gaza
Katika kuuhami na kuunga mkono utawala wa Israel, Marekani kwa mara nyingine tena imelipigia kura ya turufu azimio la nchi 10 wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilizotaka kutekelezwa usitishwaji vita haraka iwezekanavyo, bila ya masharti na wa kudumu katika Ukanda wa Gaza na kuachiwa mateka wote.
Nchi 14 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama wamelipigia kura ya ndio wakiunga mkono rasimu ya azimio lililopendekezwa katika kikao cha Baraza la Usalama la UN kilichofanyika Jumatano asubuhi kwa wakati wa Marekani.
Hakuna nchi yoyote mwanachama wa Baraza la Usalama ambayo haikulipigia kura azimio hilo bali Marekani peke yake imelipigia kura ya turufu azimio hilo lililopendekezwa kwa ajili ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza.
Nchi hizo 10 wanachama wa Baraza la Usalama ambazo ni Algeria, Ecuador, Japan, Msumbiji, Malta, Korea ya Kusini, Sierra Leone, Slovenia, Uswisi na Guyana zilikuwa zimewasilisha rasimu ya azimio kwa baraza hilo zikitaka kufikiwa usitishaji vita haraka iwezekanavyo, bila ya masharti na wa kudumu huko Gaza.