Magaidi wa Daesh watishia kuishambulia Uingereza
Kundi la kigaidi la Daesh limetishia kuwa London itakuwa mlengwa wa mashambulizi ya kundi hilo baada ya magaidi hao kutekeleza shambulio jingine katika kanisa moja huko Normandy kaskazini mwa Ufaransa.
Gazeti la Suny linalochapishwa Uingereza limeripoti kuwa, kundi la Daesh limesambaza picha likitishia kuishambulia London mji mkuu wa Uingereza na miji mikuu mingine muhimu duniani.

Vitisho hivyo vya Daesh vimetolewa masaa kadhaa baada ya askari usalama wa Uingereza kutahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini na kueleza kuwa, si jambo lililo mbali kutekelezwa mashambulizi ya kigaidi huko Uingereza.
Polisi dhidi ya ugaidi ya Uingereza imetoa maagizo maalumu kwa makanisa yote nchini na kuyatahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea tukio sawa na lile la Ufaransa.
Wakati huo huo Bi Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza amesema baada ya tukio hilo kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini humo.
