Huduma mpya za Trump kwa utawala wa Kizayuni wa Israel
Katika siku za mwanzo za muhula wake wa pili wa uongozi, Donald Trump, rais mpya wa Marekani, kwa mara nyingine tena amefuata njia ile ile aliyopitia katika muhula wa kwanza wa uongozi wake. Katika muhula wa kwanza, Trump alitoa uungaji mkono mkubwa na ambao haujashuhudiwa kwa utawala wa Kizayuni na kuchukua hatua mpya sambamba na kuiunga mkono Israel na kuwapinga Wapalestina. Vitendo na misimamo hii imekutana na majibu chanya kutoka Tel Aviv.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemshukuru Rais wa Marekani Donald Trump kwa kuondoa vikwazo vya kupeleka silaha Israel. Netanyayu ameonekana katika mkanda wa video akisema kuwa, anamshukuru Trump kwa kutekeleza ahadi yake ya kudhamini suhula na nyenzo za lazima kwa Israel ili iweze kujilinda na kuwashinda maadui wao wa pamoja.
Serikali ya Washington imesema kuwa, mabomu 1,800 ya MK-84 yaliyohifadhiwa Marekani yatasafirishwa na kupelekewa utawala wa Kizayuni wa Israel katika siku chache zijazo.
Ikulu ya White House imeiagiza Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon kuondoa kizuizi cha upelekaji wa mabomu hayo yenye uzani wa pauni 2,000 kwa Israeli, kulingana na maafisa watatu wa Israeli wanaozungumza na Axios.
Uamuzi wa Rais Joe Biden wa kusitisha usafirishaji wa mabomu hayo mwezi Mei mwaka jana uliibua mgogoro mkubwa katika uhusiano wa Marekani na Israel, wakati wa vita dhidi ya Gaza vilivyodumu kwa zaidi ya miezi 15.
Siku ya Jumamosi, Trump alisema kuwa, mambo mengi ambayo Israel iliomba hapo awali kutoka Marekani sasa yatawasilishwa kwa Tel Aviv. Kabla ya hapo Marekani ilitangaza, Trump akiwa na lengo la kuiunga mkono Israel amefuta marufuku iliyokuwa imewekwa ya kusimamisha utumaji wa mabomu yenye uzani wa pauni 2,000 kwa Israel. Usitishaji huo ulitangazwa na kutekelezwa katika kipindi cha uongozi wa Joe Biden.
Utawala wa Biden ulidai kwamba, eti una wasiwasi juu ya matumizi ya Israel ya mabomu hayo aina ya MK-84 dhidi ya Gaza yenye wakazi wengi yangelisababisha vifo vingi vya raia.
Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel, Benjamin Netanyahu na wafuasi wake huko Israel na Marekani walitumia uamuzi wa Biden kutoa madai ya nuongozo kwamba Marekani ilikuwa imeiwekea Israel vikwazo vya silaha.
Uamuzi huo wa Biden pia uliibua ukosoaji mkubwa kutoka kwa jamii ya Kiyahudi nchini Marekani ambayo kikawaida ina mwelekeo zaidi kwa Wademokrat.
Hata hivyo, kama ilivyotabiriwa, Rais mpya wa Marekani Donald Trump alihitimisha hilo ili kuutumikia utawala wa Kizayuni na kutoa kila aina ya misaada ya kijeshi kwa Israel mwanzoni mwa kipindi chake cha urais.
Suala jingine lililoibuliwa na Donald Trump katika fremu ya malengo makuu ya Israel kuhusu Ukanda wa Gaza yaani kuwaondoa Wapalestina na kuwapeleka walowezi wa Kizayuni katika eneo hilo, ni suala la kuwafukuza Wapalestina wanaoishi Gaza na kuwapeleka katika nchi nyingine.
Katika kauli zenye utata, kwa kile kinachoitwa kutatua matatizo ya Gaza, Trump ametoa wito wa kubakia tupu kikamilifu eneo hilo na Wapalestina kupatiwa makazi katika nchi jirani za Kiarabu. Trump sambamba na kuashiria kukosekana mazingira mwafaka ya kuishi, alitoa wito kwa nchi jirani za Kiarabu za maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Misri na Jordan na kutoa amri ya kuwakaribisha watu wa Gaza na kuwapa makazi ili kupunguza matatizo katika eneo hilo kwa kisingizio cha kuwahamisha wakaazi wa Ukanda wa Gaza.
Trump sambamba na kusisitiza pendekezo lake la maagizo kwa viongozi wa Misri na Jordan, amewataka washirikiane katika utekelezaji wa mpango huu.
Pamoja na hayo mpango huu wa Trump umekabiliwa na upinzani mkali wa ndani na nje ya Marekani. Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham amesema: Wazo la Donald Trump la kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza hadi mahali pengine halionekani kuwa la kutekelezeka.
Amebainisha kwamba, kwa maoni yangu, nchi za Kiarabu hazitaunga mkono mpango wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza na kuwapeleka katika nchi zingine.
Pia nchi jirani na Palestina inayokaliwa kwa mabavu zimepinga vikali ni ombi la Trump la kuwahamisha wakaazi wa Gaza hadi nchi jirani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan Ayman al-Safadi alisisitiza:
Upinzani wetu dhidi ya watu kuhamishwa na kuwafanya wakimbizi daima haubadiliki, na ni muhimu ili kufikia utulivu na amani tunayoitaka sote. Katika taarifa yake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri hapo awali iliona kuwa, kuhamishwa kwa Wapalestina na kuwaondoa wakaazi wake wa awali katika ardhi ya Palestina ni jambo lisilokubalika.
Katika muhula wa kwanza wa urais wa Donald Trump, Marekani ilichukua misimamo na hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika kuupendelea utawala wa Kizayuni. Kwa hakika, mojawapo ya matukio ya wazi ya mtazamo wa nje wa Trump ni nafasi yake katika uwanja wa uungaji mkono usio na masharti kwa Israel na utekelezaji wa hatua ambazo marais waliopita wa Marekani walikataa kuyafanya.
Muhimu zaidi kati ya hayo ni kutambuliwa kwa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kutambua kunyakuliwa miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na kuunganishwa na Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kupendekezwa ‘Muamala wa Karne” ambapo mipango yote hii imetoa upendeleo ambao haujawahi kushuhudiwa kwa Israel na wakati huo huo kuwapokonya Wapalestina haki zao za kimsingi na za wazi.
Filihali kwa kutoa idhini ya kutumwa mabomu ya pauni 2,000 kwa utawala wa Kizayuni na kuchukua msimamo ulioratibiwa na Tel Aviv kuhusu kuwafukuza Wapalestina kutoka ukanda wa Gaza, Trump anaelekea katika mkondo uleule aliopitia katika muhula wake wa kwanza wa urais wa kuhudumia utawala wa Kizayuni wa Israel.