Taasisi ya Wanafikra ya Marekani: Trump hawezi kuishinda Ansarulllah ya Yemen
(last modified Sat, 29 Mar 2025 10:46:39 GMT )
Mar 29, 2025 10:46 UTC
  • Taasisi ya Wanafikra ya Marekani: Trump hawezi kuishinda Ansarulllah ya Yemen

Taasisi ya Kutetea Demokrasia (FDD) nyenye makao yake makuu huko Washington DC imezungumzia kushindwa serikali ya Donald Trump katika kukabiliana barabara na harakati ya Ansarullah ya Yemen na kusisitiza kuwa: Serikali ya Trump inakabiliwa na hitilafu kubwa za ndani kuhusu Yemen, na muhimu zaidi, kuhusiana na Iran; na jambo hii ni moja ya sababu inayoikwamisha Marekani kuibuka na ushindi huko Yemen.

Timu ya Rais wa Marekani Donald Trump imegawanyika na kukumbwa na hitilafu kubwa kuhusu namna ya kushughulikia kadhia ya nyuklia ya Iran; ambapo kwa upande mmoja, kambi ya J.D Vance, Makamu wa Rais wa Marekani, imekuwa na msimamo wa Kihafidhina zaidi kuhusu mazungumzo ya Mashariki ya Kati na hata misimamo ya Israel dhidi ya Iran, jambo ambalo linaweza kuitumbukiza Marekani katika mgogoro; na katika upande wa pili kuna kambi ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegsett ambaye ana mtazamo wa kihasama kuhusu Yemen unashabihiana zaidi na ule wa Trump.  

Uchambuzi wa Foundation for Defense of Democracies unaeleza kuwa, Vance na waungaji mkono wake katika serikali ya Marekani wanataka Marekani ichukue hatua za kiwango cha chini, na hatua za juu zitekelelezwe na waitifaki wa Washington, na kwamba hatua hizo zisifikie kiwango cha kuilazimisha Marekani kuingia vitani. Mkabala wake, inaendelea kusema FDD, msimamo wa Hegsett na watu wa karibu yake unaonyesha kuwa wana nia ya kupanua nguvu na udhibiti wa  Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati kwa ajili ya kuilinda Israel.

Mwandishi wa uchambuzi huu ameongeza kuwa Mashariki ya Kati ni eneo la aina yake, na kwamba mwelekeo wa Trump wa kuwaacha mkono waitifaki wa jadi wa Marekani na kuepuka kuingia katika vita vya muda mrefu unakwenda sambamba na misimamo ya makamu wake.