Kupinga Uyahudi: Kisingizio cha Trump kwa ajili ya kuweka mashinikizo kwa vyuo vikuu
(last modified Sat, 05 Apr 2025 03:14:37 GMT )
Apr 05, 2025 03:14 UTC
  • Kupinga Uyahudi: Kisingizio cha Trump kwa ajili ya kuweka mashinikizo kwa vyuo vikuu

Maafisa wa serikali ya Marekani wametangaza kuwa utawala wa Donald Trump utaangalia upya bajeti ya dola bilioni 9 ya Chuo Kikuu cha Harvard kufuatia madai ya chuki dhidi ya Wayahudi kwenye chuo hicho.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Huduma za Umma ya Marekani imesema: Maafisa wa nchi hiyo watapitia mkataba wa dola milioni 255.6 kati ya Harvard na serikali, na mkataba wa dola bilioni 8.7 wa miaka mingi kwa chuo kikuu hicho maarufu.

Taarifa hiyo ilisema hatua hiyo ni sehemu ya majukumu ya Jopo Kazi la kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi. Hapo awali pia hatua kama hiyo ilichukuliwa dhidi ya Chuo Kikuu cha Columbia.

Tangu mwanzoni mwa muhula wake wa pili wa urais, Rais Donald Trump wa Marekani sanjari na misaada na himaya yake isiyo na masharti kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika nyanja za kiutamaduni na kijamii, pia amechukua hatua za kuiunga mkono na kuisaidia Israel na kuwapiga vita Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na vyuo vikuu na wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina ndani ya Marekani.

Chuo Kikuu cha Harvard pia ni miongoni mwa vyuo vilivyotangaza rasmi upinzani wao dhidi ya siasa za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wakati wote wa vita vya maangamizi ya kizazi ya Wapalestina, na wanafunzi wa chuo hicho wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kuchukuliwa hatua dhidi ya jinai za Israel. Ijapokuwa matakwa ya wanafunzi wa Harvard na kauli mbiu zao zililaaniwa na Rais wa wakati huo wa Marekani, Joe Biden, lakini Trump sasa analenga rasmi Chuo Kikuu cha Havard na vyuo vikuu vingine ambavyo wanafunzi wao walifanya maandamano ya kuitetea Palestina na kulaani mauaji ya kimbari ya Israel, na ametishia kukata au kupunguza ufadhili na bajeti ya Federali kwa vyuo hivyo. Maafisa wa uhamiaji wa Marekani pia wanafanya mikakati ya kuwatimua wanafunzi wa kigeni wanaoandamana dhidi ya mauaji ya kimbari ya Israel, wakiwemo wale wenye kadi za kijani na vibali halali vya kuishi Marekani.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Havard wakionyesha mshikamano na Palestina 

Hatua na mashinikizo hayo ya Trump kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kisingizio cha eti chuki dhidi ya Wayahudi, vinakuja wakati ambapo maafisa wa serikali ya Marekani wamekuwa wakidai kutetea uhuru wa mtu binafsi na wa kisiasa katika nchi hiyo na kuheshimu misingi ya demokrasia, lakini sasa wametupilia mbali kauli mbiu zote kwa sababu tu ya kuiunga mkono Israel na wamepitisha rasmi sera ya adhabu na kukandamiza uhuru wa kujieleza na uhuru wa kifikra na wanafunzi wa vyuo vikuu wanaotumia uhuru huo wa kikatiba. Katika muktadha huo, hivi majuzi Trump alitangaza rasmi kwenye mtandao wa kijamii kwamba, bajeti yote ya serikali kwa chuo au shule inayoruhusu maandamano haramu, itasitishwa.

Ayanna Presley, mbunge wa chama cha Democratic kutoka jimbo la Massachusetts la Marekani, anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wanawatisha wanafunzi ili kunyamazisha maandamano; Hivi ndivyo anavyofanya dikteta.

Trump anadai kuwa watetezi wa watu wa Palestina huko Marekani wana chuki dhidi ya Wayahudi. Trump amewapachika wapinzani wanaopinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Palestina kuwa ni “wafanya ghasia walioajiriwa” na kudai kuwa, wengi kati ya waandamanaji hao si wanafunzi bali ni wahuni wanaofanya vitendo hivyo ili kujipatia fedha.

Pamoja na hayo, himaya na uungaji mkono wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani kwa Wapalestina na upinzani wao dhidi ya sera za mauaji ya kimbari za Israel bado unaendelea, na suala hili limeenea sio tu katika vyuo vikuu bali pia katika jamii ya Marekani. Katika muktadha huu, mwandishi na mtafiti wa Israel, Shuki Friedman amesema katika makala yake akizungumzia kuporomoka kwa kiasi kikubwa uungaji mkono wa umma wa Marekani kwa Israel kwamba: “Licha ya msimamo wa Rais Donald Trump wa kuzidi kuihami na kuisaidia Israel, hali halisi nje ya Ikulu ya White House ni tofauti. Miongoni mwa maoni ya umma wa Marekani, uungaji mkono kwa Israel unaendelea kupungua na uungaji mkono kwa Wapalestina unaongezeka.”

Alaa kulli hal, japokuwa Trump kwa sasa anajaribu kunyamazisha harakati za wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina kupitia vitisho na mashinikizo, na anakabiliana na vyuo vikuu kwa kupunguza bajeti za taasisi hizo za elimu, lakini inaonekana kuwa wimbi la chuki dhidi ya Uzayuni miongoni mwa wanafunzi wa Marekani sio tu kwamba linazidi kushika kasi, bali pia vitendo hivyo vya Trump vinachochea zaidi hasira ya umma katika jamii ya Marekani.