Waandamanaji Paris watoa wito wa kususia utawala katili wa Israel
(last modified Sat, 17 May 2025 02:49:20 GMT )
May 17, 2025 02:49 UTC
  • Waandamanaji Paris watoa wito wa kususia utawala katili wa Israel

Maandamano ya kuunga mkono Palestina yamefanyika karibu na Wizara ya Utamaduni ya Ufaransa jijini Paris, yakitoa wito wa kususia utawala wa Israeli kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Waandamanaji waliokuwa na hasira wametoa wito wa kususia kabisa bidhaa zote kutoka Israel, wakielezea ghadhabu yao dhidi ya vitendo vya kikatili vya jeshi la Israel.  Aidha wamelaani tena mzingiro unaoendelezwa ba Israel dhidi ya Gaza ambao sasa umeingia mwezi wake wa tatu — mzingiro ambao Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameutaja kuwa “wa aibu” mapema wiki hii.

Lengo la pili la maandamano haya lilikuwa kuitaka serikali ya Ufaransa iingilie kati na kufuta tamasha la muziki lililopangwa kufanywa na mwimbaji kutoka Israel, Eyal Golan, anayewakilisha utawala huo haramu.

Wanaharakati wamesema wanapinga ujio wake, onyesho lake, na wanataka serikali ya Ufaransa ichukue hatua ya kuzuia tamasha hilo.

Golan, ambaye waandamanaji wanamshutumu kuwa mfuasi wa sera za mauaji ya kimbari zinazotekelezwa na Israel dhidi ya raia wa Gaza, anatarajiwa kufanya tamasha wiki ijayo katika mji mkuu wa Ufaransa.

Olivia Zemor kutoka shirika la Europalestine linalounga mkono mapambano ya Wapalestina kwa ajili ya ukombozi amesema: “Tumegundua kuwa kuna mwimbaji wa Kizayuni anayetetea wazi wazi mauaji ya kimbari, ambaye amesema kwa maneno yake mwenyewe kuwa Wapalestina wote wa Gaza wanapaswa kuangamizwa, wasibaki hata mmoja.”

Kinachochochea zaidi hasira za wanaharakati ni taarifa kuwa mapato ya tamasha hilo yatatumika kuchangia shirika la Magen David Adom la Israel, shirika ambalo kisheria ni la huduma za dharura, lakini waandamanaji wanasema ni sehemu ya mfumo wa kijeshi wa Israeli.

Waangalizi wanaamini tamasha hilo litaendelea kama ilivyopangwa, lakini chini ya ulinzi mkali kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kufanya maandamano nje ya ukumbi huo.

Maandamano haya ya karibuni yanalenga pia utamaduni wa Israeli sambamba na siasa zake; sera ambazo wananchi wa Ufaransa wanasema ni mkakati wa makusudi wa kuihangaisha na kuiangamiza Gaza kwa njaa hadi watu wake wakubali kupokonywa ardhi yao.