Sababu za Kuzidi Kuporomoka Umaarufu wa Israel Mbele wa Wamarekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137888-sababu_za_kuzidi_kuporomoka_umaarufu_wa_israel_mbele_wa_wamarekani
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Kituo cha Utafiti wa Maoni ya Umma cha Pew, yanaonyesha kuwa umaarufu wa Israel mbele ya tabaka la vijana wa chama cha Democrat nchini Marekani umepungua kwa asilimia 31 na mbele ya vijana wa Republican kwa asilimia 22 kulinganisha na ilivyokuwa miaka minne iliyopita.
(last modified 2026-04-22T05:05:41+00:00 )
Apr 22, 2026 04:55 UTC
  • Sababu za Kuzidi Kuporomoka Umaarufu wa Israel Mbele wa Wamarekani

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Kituo cha Utafiti wa Maoni ya Umma cha Pew, yanaonyesha kuwa umaarufu wa Israel mbele ya tabaka la vijana wa chama cha Democrat nchini Marekani umepungua kwa asilimia 31 na mbele ya vijana wa Republican kwa asilimia 22 kulinganisha na ilivyokuwa miaka minne iliyopita.

Manung’uniko, hasira na chuki dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel miongoni mwa idadi kubwa ya Wamarekani vimeshamiri kiasi kwamba hata rais wa nchi hiyo ameukiri ukweli huo.
"Iwe watu wanaipenda Israel au hawaipendi, imethibitisha kuwa ni mshirika mkubwa wa Marekani," hivyo ndivyo alivyoeleza Donald Trump kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social. 
Trump ameweka andiko hilo baada ya chungzi kadhaa za maoni kuonyesha kuwa nyota ya umaarufu wa utawala wa kizayuni mbele ya vijana wa Marekani imefifia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Wakati uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na Kituo cha Utafiti cha Pew unaonyesha kuwa umaarufu wa Israel mbele ya vijana Wademocrat umepungua kwa 31% na mbele ya Warepublican kwa 22% kulinganisha na miaka minne iliyopita, tovuti ya habari ya Axios imetahadharisha kuwa, kuporomoka umaarufu wa Israel mbele ya vijana wa Marekani kutaathiri matokeo ya uchaguzi wa bunge, na kwamba wabunge wanaiounga mkono Tel Aviv, hivi sasa wanabadilisha misimamo yao ili waweze kupata uungaji mkono wa wapiga kura. 
Kubadilika kwa mtazamo wa tabaka la vijana ndani ya Marekani kuhusiana na Israel kumetokana na sababu kadhaa. Sababu ya kwanza ni kwamba, hisia za kupinga vita na chuki dhidi ya umwagaji damu na mauaji ya kimbari zimepata nguvu zaidi miongoni mwa vijana wa Marekani kulinganisha na makundi mengine ya jamii ya nchi hiyo. Hii ni katika ambayo, katika miaka ya hivi karibuni utawala dhalimu wa Kizayuni umeonyesha bila ya hofu, tena mbele ya macho ya walimwengu aina ya kutisha na ya ukatili ya vita, mauaji ya kinyama, mauaji ya kimbari na jinai na uhalifu wa kivita nadra kuwahi kushuhudiwa. Mauaji ya halaliki ya zaidi ya watu 70,000 huko Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na hata watoto wachanga, yameamsha hisia kali za ghadhabu na chuki duniani kote ikiwemo pia ndani ya Marekani. Maandamano ya upinzani ya wanafunzi katika baadhi ya vyuo vikuu mashuhuri vya Marekani wakati wa vita vya Ghaza yalionyesha ni kwa kiwango gani vijana kwa ujumla na hasahasa tabaka la wasomi nchini Marekani lilivyochukizwa na kughadhibishwa na moto wa vita na jinai za kinyama zinazofanywa na utawala wa kizayuni. 

Maandamano ya kuunga mkono Palestina mbele ya White House

 

Lakini sambamba na hayo, nukta nyingine muhimu ni kushuhudiwa mabadiliko katika vizazi vya Wamarekani, ambapo kinyume na wazee, vijana wa nchi hiyo hawaonyeshi kuathiriwa na hisia za mihemko walizonazo wazazi wao au mababu zao kuhusiana na mauaji ya Mayahudi yanayojulikana kama Holocaust na wala hawajihisi kama wana fadhila za kulipa kwa uzayuni wa dunia, vuguvugu linalodai kuwa, kutokana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa dhidi ya Mayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, inajuzu kwa Israel kufanya mauaji kama hayo dhidi ya watu wengine. 
Kwa upande mwingine, uingiliaji wa mara kwa mara wa Israel kwa sura ya kuainisha mwelekeo wa sera za nje za Marekani kupitia lobi zake za ushawishi ndani ya nchi hiyo, au hata kudhibiti maoni ya umma vimeikasirisha sehemu kubwa ya jamii ya Wamarekani. Suala hili linapata umuhimu zaidi kutokana na umma wa Wamarekani, hususan vijana, kuielekezea kidole cha shutuma Israel za kubeba dhima ya uanzishaji vita visivyo na mwisho inavyopigana nchi yao katika eneo la Asia Magharibi. Mfano wa hivi karibuni zaidi ni kwamba akthari ya Wamarekani wanaamini kuwa, Trump ameanzisha vita dhidi ya Iran kwa mashinikizo ya Netanyahu na hasahasa kwa ajili ya kufanikisha malengo ya kujipanua ya Israel; vita ambavyo sio tu vimegharimu roho za Wamarekani, lakini pia vimepelekea kuongezeka kwa kiwango kikubwa bei za bidhaa nchini Marekani na kuwabebesha mzigo wa gharama za maisha raia wa nchi hiyo.
Mjumuiko wa sababu zote hizo umepelekea kutetereka mno nafasi ya Israel mbele ya maoni ya umma nchini Marekani. Katika hali kama hiyo, Trump anajaribu kushawishi na kuyakinaisha maoni ya umma ndani ya Marekani yaamini kwamba, hata kama Israel haishabikiwi tena nchini humo lakini ni mshirika wa Marekani. Hii ni katika hali ambayo, akthari ya Wamarekani  wanaitakidi kuwa huyo aitwaye "mshirika", badala ya kuwa na msaada kwa Marekani amekuwa zaidi ni mzigo wa kuibebesha gharama nchi hiyo; na yeye Trump pia, ameifanya kauli mbiu ya "Israel Kwanza" kuwa mbadala wa kauli mbiu yake ya "Marekani Kwanza"; muelekeo ambao, umezidi kukoleza moto wa hasira za Wamarekani…/