Mchungaji UK: Uislamu uko karibu na Issa AS zaidi kuliko Ukristo
(last modified Mon, 22 Feb 2016 03:36:20 GMT )
Feb 22, 2016 03:36 UTC
  • Mchungaji Steve Chalke
    Mchungaji Steve Chalke

Mchungaji mmoja nchini Uingereza amesema kuwa, mafundisho ya Kiislamu yako karibu na yale aliyoyafunza Yesu yaani Nabii Issa AS, kuliko mafundisho mengi yanayotolewa katika Makanisa ya Magharibi.

Mchungaji Steve Chalke, Padri na Muasisi wa Kanisa la Oasisi Charity ameliambia jarida la Christian Today kuwa, mafundisho sahihi ya kumjua Mungu yanaweza kuonekana kupitia Nabi Issa na kwamba yale aliyoyafunza Nabii huyo wa Mwenyezi Mungu yanaenda sambamba na mafundisho ya Uislamu.

Akizungumza katika uzinduzi wa kitabu chake chenye anwani isemayo “Waislamu na Wakristo wanaabudu Mungu sawa” amesema kuwa, uchunguzi wake wa muda mrefu umebaini kuwa, dini mbili hizo zinaamini uwepo wa Mungu Mmoja ingawa zinatofautiana juu ya namna ya kumuabudu.

Kiongozi huyo wa Kikristo nchini Uingereza ameongeza kuwa, “Iwapo tunasema Uislamu ni dini ya uovu na kwamba wanaabudu Mungu tofauti na Wakristo; na iwapo tunadai kuwa Ukristo ndio njia pekee ya kumpeleka mtu Peponi, basi tujue kuwa tunaelekea katika Vita vya Tatu vya Dunia.”

Mchungaji Schalke amevikosoa vyombo vya habari vya Magharibi ambavyo vinaeneza propaganda zisizo na mantiki kuuhusu Uislamu huku akisisitiza kuwa: “Tatizo ni kwamba hatuwajui Waislamu, kila mmoja anawaogopa wafuasi wa dini hiyo na tunakwepa kuwa karibu nao ghairi ya mtu jirani yake au mfanyakazi mwenzake.”