IAEA yathadharisha kuhusu uwezekano wa kushambuliwa taasisi za nyuklia
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ametahadharisha kuhusu hatari ya kushambuliwa taasisi za nyuklia.
Yukia Amano ambaye alikuwa akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Nyuklia mjini Vienna huko Austria amesema kuwa, magaidi na wahalifu wanafanya njama za kutumia vibaya dosari yoyote katika mfumo wa usalama wa nyuklia duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ameongeza kuwa, mashambulizi ya kigaidi pia yanaweza kulenga taasisi na mada za radioactive wakati wa kusafirishwa. Amano ametoa wito wa kupewa kipaumbele zaidi mazingira ya kusindika na kusafirishwa mada za radioactive zilizokwisha tumika.
Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Nyuklia ulianza jana katika makao makuu ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki mjini Vienna. Ajenda kuu ya mkutano huo ni kujadili njia za kuzuia uharibifu wa aina yoyote katika taasisi za nyuklia, kuzuia wizi wa mada za atomiki na kukabiliana na magendo ya mada za nyuklia ili zisifike kwenye mikono ya makundi ya kigaidi.