Malaysia: Serikali ya Myanmar ikomeshe jinai dhidi ya Waislamu
Waziri Mkuu wa Mayalsia, Najib Razak sambamba na kuituhumu serikali ya Myanmar kwa kuhusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, amebainisha wasi wasi wake mkubwa juu ya mgogoro wa kibinaadamu unaowakabili Waislamu wa mkoa wa Rakhine wa nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Razak ameyasema hayo leo katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Kuala Lumpur, mji mkuu wa kibiashara wa Malaysia kilichoitishwa kwa ajili ya kuchunguza hali ya Waislamu wa Myanmar ambapo sanjari na kuashiria kuwa hii leo watu wengi wa nchi hiyo wanauawa na wengine wengi kupoteza makazi yao, amesema kuwa, suala hilo limegeuka na kuwa janga linaloukabili usalama na amani ya eneo zima.

Katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Anifah Aman amesema kuwa, kwa miaka mingi sasa Waislamu wa eneo la Rakhine wamekuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa na kwamba, bila shaka kutofuatiliwa suala hilo kunatishia usalama na amani ya eneo. Kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Kuala Lumpur kwa ajili ya kuchunguza hali mbaya ya Waislamu wa Myanmara na mabadiliko ya Palestina, kimehudhuriwa na wawakilishi wa nchi 57 wanachama wa jumuiya hiyo.

Hatua mpya ya mgogoro wa Waislamu wa Rohongya nchini Myanmar, iliibuka mwezi Oktoba mwaka jana baada ya vituo kadhaa vya polisi kushambuliwa na watu wasiojulikana huko karibu na mpaka wa nchi ya Bangladesh. Baada ya tukio hilo, polisi walianzisha hujuma mtawalia dhidi ya jamii ya Waislamu sambamba na kuteketeza moto nyumba zao, suala ambalo limeifanya jamii ya kimataifa kulaani vikali ukatili huo. Hii ni katika hali ambayo Waislamu sanjari na kulaani hujuma dhidi ya vituo vya polisi, walikadhibisha tuhuma zilizoelekezwa kwao, na kuongeza kuwa hujuma hizo zilitekelezwa kwa lengo maalumu la kuhalalisha jinai na ukatili dhidi yao.