Jan 31, 2017 13:24 UTC
  • Misikiti yafungwa Uholanzi kufuatia shambulizi la Quebec, Canada

Misikiti minne ya Jamia nchini Uholanzi inatazamiwa kufungwa kutokana na kushadidi chuki dhidi ya Waislamu, siku mbili baada ya shambulizi la kikatili dhidi ya msikiti na kituo cha kidini mjini Quebec nchini Canada.

Uamuzi huo umetolewa na Maimamu na wasimamizi wa misikiti nchini Uholanzi, baada ya kufanya kikao cha dharura cha kujadili mustakabali wa maeneo hayo ya ibada kufuatia kushambuliwa waumini wa Kiislamu waliokuwa wakisali katika msikiti mmoja huko Quebec nchini Canada usiku wa kuamkia jana Jumatatu.

Said Bouharrou, afisa wa Baraza la Misikiti nchini Uholanzi (RMMN) amesema kuwa, misikiti ya Jamia katika miji ya Amsterdam, The Hague, Rotterdam na Utrech nchini humo itafungwa kwa kuhofia usalama wa waumini.

Amesema shambulizi kama la Quebec linadhihirisha jinsi chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu imeongezeka katika maeneo mbali mbali duniani na kwamba wakati umefika hatua za tahadhari zichukuliwe.

Nje ya msikiti wa Quebec Canada

Kwa mujibu wa takwimu za polisi nchini Uholanzi, chuki dhidi ya Uislamu nchini humo imeongezeka kwa kiwango cha kutia wasi wasi, ambapo mwaka juzi pekee 2015, visa zaidi ya 445 vilirekodiwa.

Mohamed Yangui, Rais wa Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec amesema waumini sita wa Kiislamu waliuawa walipokuwa wakisali Sala ya Ishaa juzi usiku, baada ya wavamizi kuvamia msikiti huo na kuwamiminia risasi ovyo. 

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani shambulizi hilo dhidi ya msikiti na kulitaja kuwa hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu.

 

Tags