100 waaga dunia kutokana na maporomoko ya theluji Afghanistan, Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24759-100_waaga_dunia_kutokana_na_maporomoko_ya_theluji_afghanistan_pakistan
Makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na maporomoko ya theluji katika nchi za Afghanistan na Pakistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2017 04:15 UTC
  • 100 waaga dunia kutokana na maporomoko ya theluji Afghanistan, Pakistan

Makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na maporomoko ya theluji katika nchi za Afghanistan na Pakistan.

Hafiz Abdul Qayum, Gavana wa mkoa wa Afghanistan Magharibi amesema kuwa watu zaidi ya 50 wamefariki dunia na makumi ya wengine kutoweka baada ya mlima wa theluji kuporomokea makazi ya watu jana Jumapili katika kijiji cha Nuristan.

Habari zinasema kuwa, watu wengine 19 wameaga dunia katika mkoa wa kaskazini wa Badakhshan, kufuatia maporomoko hayo ya theluji. Naweed Frotan, Msemaji wa Gavana wa mkoa huo amesema kuwa, mbali na milima ya theluji kuporomokea nyumba za watu katika eneo hilo, pia ilianguka barabarani na kusababisha ajali zilizoua watu wengi.

Athari za maporomoko ya thgeluji eneo la Kashmir

Habari zaidi zinasema kuwa, wilaya 12 katika mkoa wa Badakhshab zimeathiriwa zaidi na maporomoko hayo ya theluji na kwamba, ofisi nyingi za serikali zimefungwa kutokana na hali hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa, makumi ya watu wanaripotiwa kufariki dunia kutokana na maporomoko ya theluji katika nchi jirani ya Pakistan. Syed Maghferat Shah, Mkuu wa Wilaya ya Chitral amesema kuwa, zaidi ya watu 20 wameaga dunia na kujeruhiwa kutokana na janga hilo la kimaumbile katika eneo hilo, kaskazini mwa Pakistan.

Aidha shughuli zimekwama katika kituo cha upekuzi katika mpaka wa Pakistan-Afghanistan kutokana na maporomoko ya theluji, huku barabara kuu ya Kabul-Kandahar ikifungwa.