Mar 15, 2017 16:26 UTC
  • Marekani yaongoza kwa kuwa na wafungwa wengi duniani

Ripoti mpya iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha kuwa idadi ya wafungwa wanaoshikiliwa katika jela za Marekani ni kubwa zaidi kuliko ya nchi zote duniani na hivi sasa kuna karibu wafungwa milioni mbili na laki tatu katika jela za nchi hiyo.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa idadi ya wafungwa walioko katika jela za Marekani ni mara tano zaidi ya idadi ya wafungwa wa nchi zenye wafungwa wengi duniani. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya wafungwa wahajiri huko Marekani pia imeongezeka. Imebainika pia kwamba kati ya kila wafungwa watano walioko katika jela huko Marekani, mfungwa mmoja amehukumiwa kifungo jela kwa kosa linalohusiana na madawa ya kulevya. 

Wafungwa katika moja ya jela za mjini Chicago Marekani 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa kuna haja ya kutazamwa upya sera ya kuendesha mapambano dhidi ya mihadarati ili kukomesha kuwepo idadi kubwa kama hiyo ya wafungwa nchini Marekani, bali pia liangaliwe upya jibu la jamii ya Marekani kuhusu vitendo vya utumiaji mabavu.  

Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya "Policy Think Tank" kuhusu wafungwa imeashiria pia kuhumiwa vifungo vya jela watoto 6,600 huko Marekani na kubainisha kuwa watu wasiopungua elfu 57 wamefungwa jela huko Marekani kwa sababu tu ya kuingia nchini humo. Aidha inatarajiwa kuwa siasa dhidi ya wahajiri za Rais Donald Trump wa Marekani zitapelekea kuongezeka idadi ya wahajiri watakaofungwa jela nchini humo. 

Tags