Pakistan yavurumisha zaidi ya makombora 70 Afghanistan, Kabul yalalamika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27086-pakistan_yavurumisha_zaidi_ya_makombora_70_afghanistan_kabul_yalalamika
Viongozi wa serikali ya Afghanistan wamesema kuwa, zaidi ya makombora 70 yalirushwa jana usiku kutoka nchini Pakistan kuelekea maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, na kuzusha wasiwasi mkubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2017 02:19 UTC
  • Pakistan yavurumisha zaidi ya makombora 70 Afghanistan, Kabul yalalamika

Viongozi wa serikali ya Afghanistan wamesema kuwa, zaidi ya makombora 70 yalirushwa jana usiku kutoka nchini Pakistan kuelekea maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, na kuzusha wasiwasi mkubwa.

Faridullah Dehqan, msemaji wa jeshi la polisi wa wilaya ya Kunar mashariki mwa Afghanistan amesema kuwa, makombora hayo yalilenga mji wa Sarkani na kusababisha uharibifu mkubwa ikiwemo wa roho na mali za watu. Mwezi uliopita pia Jumeh Gole, kamanda wa polisi wa wilaya ya Kunar alitangaza kwamba mashambulizi ya makombora ya jeshi la Pakistan katika mji huo yalisababisha hasara kubwa.

Raia wa Afghanistan wakiwa katika hali ya taharuki 

Alisema kuwa zaidi ya makombora 145 yalivurumishwa kutoka Pakistan na kuangukia katika mji wa Sarkani. Inaelezwa kuwa, mashambulizi hayo yamesababisha zaidi ya watu 1000 kuwa wakimbizi sambamba na raia kufanya maandamano makubwa kulalamikia chokochoko hizo za Pakistan dhidi ya nchi yao. Inafaa kuashiria kuwa, baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyojiri katika mji wa Sindh, jeshi la Pakistan liliweka zana za kijeshi katika mpaka wake na Afghanistan na kuanzisha wimbi la mashambulizi ya makombora dhidi ya nchi hiyo jirani.

Majeruhi wakiwahishwa hospitalini

Hata hivyo na licha ya radiamali na maandamano makubwa ya raia wa Afghanistan katika kulaani mashambulizi hayo, kwa mara nyingine jeshi la Pakistan limeendeleza mashambulizi yake nchini humo, suala ambalo limezusha wasiwasi mkubwa.