Rouhani na Putin walaani vikali mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria
Rais Hassan Rouhani wa Iran na mwenzake wa Russia Vladimir Putin wamelaani vikali hatua ya Marekani ya kukishambulia kituo cha kijeshi cha Syria kwa makombora na kusema kuwa kitendo hicho kilifanyika ili kuyapa motisha na kuyaunga mkono magenge ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika mazungumzo ya simu na Rais Putin wa Russia, Rais Rouhani amesema mashambulizi hayo ya Marekani dhidi ya Syria ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo na kwamba kuna haja ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani hujuma hiyo na kuijadili haraka iwezekanavyo.
Dakta Rouhani kadhalika amekosoa vikali hatua ya magenge ya kigaidi nchini humo kutumia silaha za kemikali na kusisitiza kuwa, hujuma hiyo ya Marekani yumkini ikayapa nguvu magenge hayo kuendelea kutumia silaha hizo haramu.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema hatua hiyo ya Marekani ya kujaribu kuyashajiisha magenge ya kigaidi nchini Syria ni jambo lisilokubalika. Kadhalika ameeleza kushangazwa kwake na kisingizo kilichotolewa na Washington cha kuhalalisha mashambulizi yake hayo na kubainisha kuwa, Umoja wa Mataifa wenyewe umewahi kukiri kuwa serikali ya Syria haimiliki silaha zozote za kemikali.
Usiku wa kuamkia Ijumaa, Marekani ilivurumisha makombora 59 kutokea katika meli zake mbili za kivita katika bahari ya Mediterania na kukishambulia kituo cha jeshi la anga la Syria katika eneo la Shayrat katika mkoa wa Homs na kuuwa watu tisa wakiwemo watoto wanne na kujeruhi wengine kadhaa.
Rais Bashar al-Assad wa Syria sambamba na kulaani chokochoko hizo za Marekani amesema kuwa, hatua ya Washington kuishambulia nchi yake ni ya kijinga na inayotokana na mtazamo finyu wa kisiasa na kijeshi.