Marekani yapiga "Mama wa Mabomu Yote", Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27744-marekani_yapiga_mama_wa_mabomu_yote_afghanistan
Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imetangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limepiga bomu kubwa zaidi lisilokuwa la nyuklia nchini Afghanistan.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 14, 2017 00:01 UTC
  • Marekani yapiga

Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imetangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limepiga bomu kubwa zaidi lisilokuwa la nyuklia nchini Afghanistan.

Ripoti iliyotolewa jana Alkhamisi na Pentagon imesema kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa jeshi la Marekani limetumia bomu lake kubwa zaidi lisilokuwa la nyuklia katika viunga vya mji wa Achin kwenye mkoa wa Nangarhar huko Afghanistan.

Taarifa ya Pentagon imesema hii ni mara ya kwanza kutumiwa bomu hilo vitani.

Bomu la MOAB ambalo pia linajulikana kwa jina la "Mama wa Mabomu Yote", lina uzito wa tani 11 za mada za milipuko ya TNT na ndilo lenye uharibifu mkubwa zaidi ya mabomu yote ya Marekani yasiyo ya nyuklia. 

MOAB, bomu lenye nguvu kubwa zaidi lisilo la nyuklia la Marekani.

Marekani imedai kuwa imetumia bomu hilo dhidi ya ngome za kundi la Daesh katika mkoa wa Nangarhar. 

Mashambulizi haya ya Marekani huko Afghanistan yamefanyika wiki moja tu baada ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump kushambulia kituo cha jeshi la anga nchini Syria. Watu kadhaa waliuawa katika shambulizi hilo.

Mwaka 2001 Marekani iliishambulia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Uvamizi huo haukuwa na faida ghairi ya kuua maelfu ya raia wa Afghanistan na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo.