Karzai aikosoa US kwa kudondosha "Mama wa Mabomu Yote" nchini Afghanistan
Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai ameikosoa vikali Marekani kwa kuitumia nchi yake kama sehemu ya kufanyia majaribio ya silaha zake.
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Karzai amesema: "Ninalaani vikali hatua ya Marekani kudondosha nchini bomu kubwa zaidi duniani lisilo la nyuklia, na kuna haja ya serikali ya Kabul kuizuia US isichukue hatua zaidi za hatari za namna hii."
Karzai ambaye alikuwa rais wa kwanza nchini Afghanistan chini ya makubaliano ya nchi za Magharibi, baada ya Marekani kuivamia kijeshi nchi hiyo mwaka 2001, amesema kitendo hicho cha Marekani hakina uhusiano wowote na vita dhidi ya ugaidi, lakini ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kujitawala Afghanistan, na ni jambo lisilokubalika kuifanya nchi hiyo kuwa sehemu ya kufanyia majaribio ya silaha zake mpya na hatari.
Mapema Alkhamisi, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilitangaza kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa jeshi la nchi hiyo limetumia bomu lake kubwa zaidi lisilo la nyuklia katika viunga vya mji wa Achin kwenye mkoa wa Nangarhar huko Afghanistan.
Bomu hilo la GBU-43B maarufu kwa jina la "Mama wa Mabomu Yote" lina uzito wa tani 11 za mada za milipuko ya TNT na ndilo lenye uharibifu mkubwa zaidi kuliko mabomu yote yasiyo ya nyuklia duniani.
Rais wa Marekani Donald Trump amepongeza operesheni hiyo dhidi ya Afghanistan na kudai kuwa makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS (Daesh) wameuawa.