Karzai: Nitaiokoa Afghanistan mwenyewe kutokana na jinai za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27810-karzai_nitaiokoa_afghanistan_mwenyewe_kutokana_na_jinai_za_marekani
Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai amesema kuwa atasimama yeye mwenyewe kukabiliana na Marekani ili kuiokoa nchi yake kutokana na jinai za Washington nchini humo.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 15, 2017 09:18 UTC
  • Karzai: Nitaiokoa Afghanistan mwenyewe kutokana na jinai za Marekani

Rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai amesema kuwa atasimama yeye mwenyewe kukabiliana na Marekani ili kuiokoa nchi yake kutokana na jinai za Washington nchini humo.

Karzai ameyasema hayo leo katika kikao mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan na kuongeza kuwa, kuanzia leo hatoitambua tena serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwa, kitendo cha Marekani cha kulifanyia majaribio bomu kubwa zaidi duniani lisilo la nyuklia katika mkoa wa Nangarhar ni kuivunjia heshima nchi hiyo.

"Mama wa Mabomu Yote" ya Marekani

Hamid Karzai amelaani hatua ya Marekani ya kufyatua bomu hilo lenye uzito wa kilo elfu 10 katika mji wa Achin na amewataka raia wa nchi hiyo kukabiliana na jinai za Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Rais huyo wa zamani wa Afghanistan amesema kuwa, hatari na athari mbaya inayotokana na hatua hiyo ya Marekani itawaathiri raia wa nchi hiyo kwa makumi ya miaka. Mapema Alkhamisi, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilitangaza kuwa, kwa mara ya kwanza jeshi la nchi hiyo limetumia bomu lake kubwa zaidi lisilo la nyuklia katika viunga vya mji wa Achin kwenye mkoa wa Nangarhar nchini Afghanistan, ambapo kutokana na bomu hilo, makumi ya watu waliuawa bila hatia. 

Raia wa kawaida wakiwemo watoto waliouawa na Marekani katika hujuma hiyo

Bomu hilo la GBU-43B maarufu kwa jina la "Mama wa Mabomu Yote" lina uzito wa tani 11 za mada za milipuko ya TNT na ndilo lenye uharibifu mkubwa zaidi kuliko mabomu yote yasiyo ya nyuklia duniani.