Taleban: Marekani imetumia silaha za kemikali katika mkoa wa Kunduz
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28128-taleban_marekani_imetumia_silaha_za_kemikali_katika_mkoa_wa_kunduz
Msemaji wa Kundi la kigaidi la Taleban amesema kuwa, Marekani imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia katika mkoa wa Kunduz, kaskazini mwa Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2017 23:52 UTC
  • Taleban: Marekani imetumia silaha za kemikali katika mkoa wa Kunduz

Msemaji wa Kundi la kigaidi la Taleban amesema kuwa, Marekani imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia katika mkoa wa Kunduz, kaskazini mwa Afghanistan.

Zabihullah Mujahid, Msemaji wa genge hilo la ukufurishaji ametangaza kuwa, katika shambulizi la silaha za kemikali lililofanyika katika eneo la Alchin katika mkoa wa Kunduz, raia kadhaa wamedhurika kutokana na hujuma hiyo.

Mujahid ameongeza kuwa, shambulizi hilo limefanyika katika operesheni za askari wa Marekani katika eneo hilo na kudai kuwa, awali wapiganaji wa kundi la Taleban walizuia kusonga mbele kwa askari hao na kuwafanya warudi nyuma. Msemaji wa genge hilo la ukufurishaji la Taleban amedai kuwa, baada ya kuwarejesha nyuma ndipo askari hao wa Marekani walipotumia silaha hizo za kemikali dhidi ya raia. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai sambamba na kusema kuwa, Marekani ndio ilioanzisha kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS), ingali inaendeleza mahusiano na kundi la kigaidi la Taleban linalofanya jinai nchini humo.

Hali baada ya kupigwa silaha za kemikali

Siku chache zilizopita pia Marekani ilipiga bomu la "Mama wa Mabomu Yote" lenye uzito wa tani 11 za mada za milipuko ya TNT na lenye uharibifu mkubwa zaidi kuliko mabomu yote yasiyo ya nyuklia duniani katika mji wa Achin mkoa wa Nangarhar ambapo raia kadhaa waliuawa bila hatia. Weledi wa mambo wanazitaja operesheni za Marekani dhidi ya kundi la Taleban huko Afghanistan kuwa ni njama tu za kutaka kuendelea kusalia ndani ya ardhi ya nchi hiyo masikini.