Abdullah Abdullah: Daesh na Taleban ndio maadui hatari sana wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28410-abdullah_abdullah_daesh_na_taleban_ndio_maadui_hatari_sana_wa_afghanistan
Mkuu wa Baraza la Utendaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan amesema kuwa, genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na Taleban ndio maadui hatari zaidi kwa taifa hilo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 29, 2017 10:52 UTC
  • Abdullah Abdullah: Daesh na Taleban ndio maadui hatari sana wa Afghanistan

Mkuu wa Baraza la Utendaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan amesema kuwa, genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) na Taleban ndio maadui hatari zaidi kwa taifa hilo.

Abdullah Abdullah ameyasema hayo leo Jumamosi katika sherehe za ushindi wa wananchi wa Afghanistan dhidi ya jeshi jekundu la Urusi ya zamani, sherehe zilizofanyika katika mji wa Panjshir kaskazini mashariki mwa Afghanistan. Amesema kuwa Waafghani wamekusudia kusimama imara katika kukabiliana na hujuma za wanamgambo wa makundi ya kigaidi  kama vile, Daesh na Taleban, ili kuliletea taifa lao usalama na amani.

Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan,

Hii ni katika hali ambayo Wizara ya Kazi na Masuala ya Kijamii nchini Afghanistan ilikuwa imeitangaza leo kuwa siku ya likizo ya kitaifa kwa mnasaba wa sherehe hizo. Inafaa kuashiria kuwa, mapambano ya wapiganaji wa mujahidina waliopambana kwa karibu miaka 14, hatimaye yalifikia ushindi kwa kuuondoa madarakani utawala wa Mohammad Najibullah mwaka 1992. 

Katika taarifa nyingine, polisi yaAfghanistan imetangaza habari ya kuangamizwa kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi la Taleban anayejulikana kwa jina la Mawlawi Daud. Taarifa hiyo imesema kwamba, kiongozi huyo wa Taleban ambaye aliwahi kuwa kamanda wa zamani wa genge hilo mjini Kabul katika kipindi cha utawala wa Taleban nchini humo, ameangamizwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Taleban

Hii ni katika hali ambayo Taleban wamelinyoshea kidole cha lawama kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) kwamba ndilo lililofanya mauaji hayo. Wakati huo huo, jeshi la Afghanistan limetangaza kuwa, limewaangamiza magaidi 45 wa kundi la kigaidi la Daesh. Kwa mujibu wa habari hiyo, magaidi hao wameuawa katika operesheni tofauti zilizofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya makundi ya kigaidi katika mkoa wa Nangarhar. Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imetangaza kuwa, magaidi hao wameuawa katika mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za kundi hilo hatari katika eneo la eneo la Achin mkoani Nangarhar.