UNICEF: Maradhi ya ukimwi yangali ni tishio duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28776-unicef_maradhi_ya_ukimwi_yangali_ni_tishio_duniani
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, bado maradhi ya ukimwi yangali ni tishio ulimwenguni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 07, 2017 13:26 UTC
  • UNICEF: Maradhi ya ukimwi yangali ni tishio duniani

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, bado maradhi ya ukimwi yangali ni tishio ulimwenguni.

Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imebainisha kuwa, kwa uchache mtoto mmoja kati ya kila watoto watano magharibi mwa Afrika hana mzazi wake mmoja ambaye ameaga dunia kutokana na maradhi ya ukimwi.

Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF iliyotolewa leo kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mayatima wa Ukimwi imeeleza kuwa, ugonjwa wa ukimwi umeendelea kuwa maradhi tishio zaidi ulimwenguni.

Ripoti zinaonyesha kuwa,  takribani watoto elfu tatu hupoteza maisha kila wiki kutokana na athari ya maambukizo ya virusi vya ukimwi huku watoto wapatao 4000 wakizaliwa kila siku wakiwa wameambukizwa virushi vya ukimwi HIV.

AIDS

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa, katika mwaka 2015 watu zaidi ya milioni mbili waliambukizwa virusi vya HIV kote duniani. Hata hiyo jambo la kutia matumaini kidogo ni kwamba, idadi ya vifo vya watu vilivyosababishwa na Ukimwi ilipungua mwaka jana ikinganishwa na mwaka 2005 na inasemekana kuwa suala hilo kwa kiasi fulani linafungamana na kuongezeka taathira za dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya wagonjwa wapya wa Ukimwi wapo katika nchi zinazostawi. Ughali wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi na gharama za afya na lishe ya watu walioambukizwa ugonjwa huo ni miongoni mwa matatizo yaliyopo katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo katika nchi zinazostawi.