Kofi Annan amtaka Trump aache misimamo ya chuki dhidi ya Iran
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa Rais wa Marekani Donald Trump kufanya mazungumzo na Iran badala ya kushikilia misimamo yake ya uhasama dhidi ya Tehran.
Kofi Annan ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, kuna haja Trump atafute njia ya kufanya mazungumzo na Iran na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ni sehemu ya suluhu ya migogoro inayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo Syria na Iraq.
Dakta Annan sambamba na kupongeza ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi wa Iran, amesema hatua ya Iran kufikia makubaliano ya historia ya nyuklia mwaka 2015, ni ithibati kuwa taifa hilo linafadhilisha uhusiano mzuri na wa amani na ulimwengu wa nje.
Katibu Mkuu wa zamani wa UN amesema: "Sielewi ni kwa nini Trump hawezi kwenda Iran, lakini alitangaza kuwa yuko tayari kukutana na viongozi wa Korea Kaskazini ilihali Tehran imeonyesha nidhamu na uwajibikaji kuliko Pyongyang."
Katika safari yake ya kwanza nje ya nchi huko Saudi Arabia na Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Trump kama alivyofanya wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, aliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaunga mkono ugaidi, ikiwa ni muendelezo wa uchochezi dhidi ya Tehran na kuifanya ichukiwe na kuogopwa katika eneo hili muhimu la Mashariki ya Kati.