Jun 05, 2017 14:22 UTC
  • HRW yalaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali jinai, ukandamizaji, ubaguzi na ukaliwaji wa mabavu wa ardhi za Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa zaidi ya miongo mitano sasa.

Shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Marekani limeyasema hayo kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 50 wa ukaliaji mabavu kikamilifu mji wa Quds kufuatia vita vya siku sita na nchi za Kiarabu.

Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema Wapalestina wamepitia kipindi kigumu cha jinai za Israel kwa muda wa miaka 50 katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wanawake wa Kipalestina wakiandamana kulaani jinai za Israel, Gaza

Amesema: "Miongoni mwa jinai hizo ni pamoja na watoto wa Kipalestina kuhukumiwa jela na mahakama za kijeshi au kuuawa pasina sababu yoyote ya msingi, nyumba zao kubomolewa sambamba na kuwekewa mbinyo mkali kiasi cha kunyimwa uhuru hata wa kutembea."

Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch amesema mamia ya Wapalestina waliuawa katika vita vitatu vya Israel dhidi ya Gaza mwaka 2008, 2012 na 2014, mashambulizi ambayo yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu na mengine ni jinai za kivita.

Tangu mwaka 2007 hadi sasa, utawala wa Kizayuni wa Israel umeuwekea mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu Ukanda wa Gaza unaoambatana na vikwazo na vizuizi vikali.

 

Tags