Bunge la Ujerumani laruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31234-bunge_la_ujerumani_laruhusu_ndoa_za_watu_wenye_jinsia_moja
Ijumaa ya juzi Bunge la Ujerumani, Bundestag liliipasisha sheria inayoruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja na kutambua rasmi eti haki watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ya kulea watoto nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 02, 2017 03:48 UTC
  • Bunge la Ujerumani laruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja

Ijumaa ya juzi Bunge la Ujerumani, Bundestag liliipasisha sheria inayoruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja na kutambua rasmi eti haki watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ya kulea watoto nchini humo.

Vyama vya Social Democratic (SPD), chama cha kushoto na chama cha kijani ambavyo vinaunda muungano wa waliowengi unaolegalega katika Bunge la Ujerumani, vilifanikiwa  kupasisha mpango wa kuruhusu ndoa za watu wenye jinsia moja katika Bunge la nchi hiyo kwa uratibu na baadhi ya Wabunge wahafidhina.

Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani ametangaza kuwa, ameupigia kura ya hapana muswaada wa sheria uliozusha mjalada mkubwa wa ndoa baina ya watu wenye jinsia moja, kwa sababu kwa mtazamo wake ndoa maana yake ni mfungamano baina ya mwanamke na mwanaume.

Licha ya upinzani wa Merkel kwa suala hilo, lakini baada ya kupita miaka minne tangu kupendekezwa mpango huo na kupingwa na vyama viwili vya Kikristo vya Christian Social na Christian Democracy, wiki iliyopita alitangaza kuwa, hili ni swali ambalo linapaswa kutolewa majibu na dhamira huru na kwa utaratibu huo akafungua njia ya kupasishwa sheria hiyo ndani ya Bunge. Kuhusiana na hilo, askofu wa mji wa Berlin ameeleza kusikitishwa kwake na kupasishwa sheria hiyo katika Bunge la Ujerumani na kusema bayana kwamba, kutekelezwa kwa sheria hiyo, kutapelekea kupungua kwa ndoa za jadi na kuhatarisha misingi na nguzo za familia. 

Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani

Licha ya kupasishwa kwa sheria hiyo, bado kuna mjadala mkali baina ya wapinzani na waungaji mkono wake kuhusiana na kuoana kwake na Katiba ya Ujerumani. Mkuu wa muungano wa vyama vya Kikristo vya Christian Social  na Christian Democracy ambaye ni miongoni mwa wapinzani wa ndoa baina ya watu wenye jinsia moja anatilia shaka juu ya kutabikiana sheria hiyo na Katiba. 

Mkabala wake, Thomas Oppermann Mkuu wa Chama cha Social Democracy sambamba na kuashiria kipengee cha sita cha Katiba ya Ujerumani kinachohusiana na dhamana ya serikali katika kuunga mkono wanandoa na familia amedai kuwa, hakuna haja ya kufanyiwa marekebisho Katiba kwa ajili ya ndoa za watu wa jinsia moja.

Licha ya kuweko hatua zilizochukuliwa na Bundestag yaani Bunge la Ujerumani kwa ajili ya kupasisha sheria ya ndoa ya watu wa jinsia moja, hiyo haina maana kwamba, jamii yote ya Ujerumani inaunga mkono uchafu huo wa kimaadili unaokinzana na maumbili ya mwanadamu. Hii ni kutokana na kuwa, kungali kunashuhudiwa kundi la wananchi wa Ujerumani wanaotaka kusitishwa mwenendo huo. Pamoja na hayo yote, haiwezekani kukanusha ukweli huu kwamba, kupasishwa sheria hiyo ni kupigwa hatua moja kubwa kurudi nyuma na bila shaka kutekelezwa sheria hiyo iliyo dhidi ya maadili na dhidi ya dini, kutaandaa uwanja wa kuenezwa ufuska na kusambaratisha misingi na nguzo za familia.

Maandamano ya kupinga mapenzi ya jinsia moja

Ukweli wa mambo ni kuwa, kupasisha sheria ya kuhalalisha maingiliano ya ngono baina ya watu wa jinsia moja kutapelekea kusambaratika utambulisho wa ndoa ukiwa kama mfungamano baina ya mwanaume na mwanamke ambao umeshuhudiwa katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu.

Katika upande mwingine kwa kuzingatia kwamba, Ujerumani ni nchi muhimu zaidi ya Umoja wa Ulaya na nchi kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya, hivyo inawezekana kutabiri kwamba, kupasishwa kwa sheria hiyo kunaweza kuzishajiisha nchi nyingine za Ulaya ambazo bado hazijatambua kisheria hiyo kuchukua hatua kuelekea katika uwanja huo. Kwa muktadha huo, jamii za Ulaya na kiujumla jamii za Magharibi zitazidi kuelekea upande wa kuporomoka kimaadili.

Hapana shaka kuwa, utendaji huo wa Wamagharibi ni kinyume kabisa na madai yao ya kubeba bendera ya ustawi na maendeleo ya jamii ya mwanadamu katika pembe mbalimbali za dunia. Wamagharibi daima wamekuwa wakisisitiza kuhusiana na kuongoza kwao kiutamaduni na kiitikadi mbele ya tamaduni na thamani nyingine na daima wamekuwa wakitoa madai ya kuzituhumu tamaduni na staarabu za wengine kwamba, zimebakia nyuma. Katika uwanja huu, katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Ulaya zilifanya juhudi za kutambuliwa rasmi haki za watu wanaojamiiana kinyume na maumbile likiwemo suala la kuhalalisha ndoa zao. Sasa Ujerumani inakuwa nchi ya 21 ya bara Ulaya kupasisha sheria ya ndoa ya watu wa jinsia moja. Denmark ndio iliyokuwa nchi ya kwanza ambayo ilipasisha sheria kama hiyo mwaka 1992.