UNICEF: Zaidi ya nusu ya wakimbizi barani Afrika ni watoto wadogo
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umesema kuwa, zaidi yawatoto milioni saba wa maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika wanaishi katika mazingira magumu kutokana na matatizo mbalimbali kama vile ukatili, umaskini na kuharibika hali ya hewa na kwamba idadi hiyo inaunda zaidi ya nusu ya wakimbizi barani Afrika.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, UNICEF imetangaza leo Jumatano kwamba, zaidi ya watoto milioni saba wa Afrika wanaishi katika kambi za wakimbizi wakiwa kwenye mazingira magumu na wanateseka kwa umaskini, ukatili wa watu waliowazidi nguvu, hali mbaya ya hewa na ukosefu mkubwa wa usalama.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF, kukosekana fursa nzuri za uchumi sahihi, ukosefu mkubwa wa amani unaotokana na vita na umwagaji damu pamoja na hali mbaya ya hewa, kumewalizimisha zaidi ya wakazi milioni 12 wa maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika kuyakimbia makazi yao.
Kwa upande wake, baraza la wakimbizi la Norway limetoa ripoti na kusema kuwa, tangu yalipoanza mapigano baina ya waasi wa Seleka na wanamgambo wa Kikristo wa Anti Balaka mwaka 2013 huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi hivi sasa, karibu watu miioni moja wamelazimika kuyakimbia maeneo yao.
Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, karibu watu milioni 65 na laki sita wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika maeneo tofauti duniani ambapo karibu nuru ya wakimbizi hao ni watoto wadogo.