Matamshi ya James Mattis; ndoto ambazo kamwe hazitatimia
James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani anasema kuwa, ili kuweko uhusiano chanya wa pande mbili kati ya Iran na Marekani, kuna ulazima wa kubadilishwa mfumo unaotawala hapa nchini.
Jenerali James Mattis ameongeza katika madai yake kwamba, Iran sio nchi ya kidemokrasia na kwamba, kila juhudi za kutaka kuanzisha uhusiano na nchi hii zitakabiliwa na vizingiti maalumu.
Aidha waziri huyo wa ulinzi wa Marekani amesema: "...Wote katika Mashariki ya Kati kuanzia Tel Aviv mpaka Cairo Misri wameeleza kwamba, Iran ni chimbuko kuu la matatizo ya eneo na kwamba, nchi hii imekuwa na taathira kubwa haribifu mkabala na uthabiti wa eneo."
Tangu huko nyuma, katika uhusiano wake na Iran, Marekani haijawa na kitu kingine bighairi ya chuki na uhasama dhidi ya wananchi wa taifa hili na hivyo kuwafanya Wairani kutoiamini hata chembe. Huko nyuma Marekani haikuwa ikiitazama Iran isipokuwa kwa jicho la Uistikbari na haikuwa ikizingatia kitu kingine katika uhusiano na taifa hili ghairi ya kujinufaisha na kusukuma mbele gurudumu la malengo yake ya kibeberu. Utawala wa wakati huo wa Iran yaani kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ulikuwa ukilinda maslahi ya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Kwa mtazamo wa Marekani utawala kama huo ulikuwa ukihesabiwa kuwa ni wa kidemokrasia. Katika zama hizo, Marekani kwa kuitegemea Saudia na utawala wa Shah iliendeleza siasa zake za kujitanua na haikuwa na wasiwasi wowote kwa Israel.
Lakini baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na taifa la Iran kusimama kidete mbele ya mfumo wa kibeberu wa Marekani na madola yote yenye kutumia mabavu, taifa hili likawa na heshima na izza, jambo ambalo liliifanya Marekani ibadilishe mtazamo wake kuhusiana na taifa hili. Katika mtazamo mpya wa Marekani ni kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao umepatikana kwa ridhaa kamili ya wananchi, sio mfumo wa kidemokrasia.
Marekani imetumia kila njia ili kutoa pigo kwa mfumo huu unaotawala nchini Iran. Kubadilishwa ubalozi wa Marekani nchini Iran katika zama hizo kuwa pango la kijasusi, kuandaliwa njama za kuusambaratisha mfumo wa Kiislamu, hujuma ya Jeshi la Marekani dhidi ya Iran katika Jangwa la Tabas, kumuunga mkono dikteta Saddam katika vita vya kulazimishwa dhidi ya taifa hili vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq, aina kwa aina ya vikwazo na kuundwa muungano dhidi ya Iran katika eneo ni sehemu tu ya mikakati ya Marekani dhidi ya taifa hili.
Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa, ugomvi wa Marekani na chuki zake dhidi ya Iran hautokani na kutokuweko demokrasia hapa nchini au masuala ya haki za binadamu. Hapana shaka kuwa, kusimama kidete Iran na kutokubali kuburuzwa na Marekani pamoja na kuwa na nafasi muhimu nchi hii katika matukio ya Mashariki ya Kati ni mambo ambayo hayaifurahishi Marekani hata kidogo.
Hivi karibuni Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA alinukuliwa akisema kuwa: Hii leo tunashuhudia kuongozeka nguvu na ushawishi wa Iran ambao ni mkubwa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma. Iran iko kila mahala katika Mashariki ya Kati.
Mike Pompeo ameongeza kuwa: Usalama wa taifa wa Marekani unakabiliwa na tishio kutoka Iran.
Tishio hilo lilianza kuzungumziwa wakati Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipovuruga mahesabu mengi ya Marekani katika Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla.
Hatua ya Iran ya kusimama kidete mkabala na siasa za Marekani za kuingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine, imelifanya taifa hili kuwa kigezo kwa nchi nyingine katika mapambano dhidi ya mfumo wa kibeberu.
Ni jambo lililo wazi kwamba, harakati hii ya Kimapinduzi imebadilisha mahesabu na kuyafanya kuwa ni kwa maslahi ya mataifa madhulumu ulimwengu hususan taifa madhulumu la Palestina. Taathira ya Iran katika miongo hii minne si tu kwamba, haijapungua, bali imekuwa ikiongezeka kila siku.