Sisitizo la Marekani la kudumisha siasa za vikwazo dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31992-sisitizo_la_marekani_la_kudumisha_siasa_za_vikwazo_dhidi_ya_iran
Vikwazo, ni neno muhimu na la msingi ambalo limekuwa likitumiwa na watawala wa Marekani katika siasa zao za chuki na uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2017 21:50 UTC

Vikwazo, ni neno muhimu na la msingi ambalo limekuwa likitumiwa na watawala wa Marekani katika siasa zao za chuki na uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baadhi ya wabunge na washauri wa masuala ya kisasa wa watawala wa Marekani wanaamini kuwa vikwazo ndiyo njia bora zaidi ya kutoa mashinikizo dhidi ya Iran. Kwa msingi huo siku ya Jumanne tarehe 18 Julai Wizara ya Fedha ya Marekani iliongeza majina 18 ya mashirika na maafisa wa Iran katika orodha ya vikwazo ya nchi hiyo kwa visingizio mbalimbali kikiwemo cha kuhusika mashirika na maafisa hao katika mpango wa makombora wa Iran. Huku ikilaani vikali hatua hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imetishia kuwawekea vikwazo maafisa wa Marekani. Kabla ya hapo tarehe 17 Mei mwaka huu, Marekani ilichukua hatua nyingine kama hiyo kwa kuwawekea vikwazo watu na mashirika saba ya Iran na China kwa tuhuma za kuhusika katika mpango huo wa makombora. Orodha hiyo ndefu ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inarejea nyuma hadi mwaka 1979 wakati wa kutekwa pango la ujasusi (ubalozi) la Marekani mjini Tehran. Tarehe 14 Novemba 1979 Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani alitoa amri ya kufungiwa pesa za Iran zilizokuwa zimewekwa katika benki za Marekani.

Jimmy Carter, rais wa zamani wa Marekani

Wakati mlipuko wa bomu ulipotokea mjini Beirut mwaka 1984 kidole cha lawama cha Marekani kilielekezewa Iran na hicho kikawa kisingizio kingine kizuri cha kuanzishwa orodha ndefu ya vikwazo dhidi ya Iran. Wakati huo Iran iliwekwa katika orodha nyingine ya nchi zinazounga mkono ugaidi kwa mtazamo wa Marekani. Katika sekta ya uwekezaji, tarehe 30 Aprili 1995, Bill Clinton, rais wa wakati huo wa Marekani alitia saini sheria iliyozuia mashirika ya Marekani kuwekeza nchini Iran. Sheria ya kuwekewa vikwazo Iran na Libya ya mwaka 1996 ni hatua nyingine ya kiuhasama iliyochukuliwa kwa ajili ya kupiga marufuku mashirika ya kigeni yasiyo ya Marekani kuwekeza katika sekta ya nishati ya Iran. Katika mzunguko huo wa vikwazo dhidi ya Iran Wizara ya Fedha ya Marekani ilipasisha vikwazo vingine vya kifedha dhidi ya Iran ambapo hata vifurushi vya zawadi vya zaidi ya dola 100 za Marekani pamoja na miamala mingine ya kifedha na mashirika ya Iran ilipigwa marufuku.

Mwishoni mwa mwaka 2011, Marekani iliyapiga marufuku mashirika na taasisi za kifedha za kigeni kufanya biashara na benki za Iran zilizowekewa vikwazo na vilevile Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kufuatia mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 mjini New York, Rais George Bush alipitisha sheria iliyoruhusu kuzuiwa fedha za watu walioshukiwa kuhusika na ugaidi.

Kutekwa pango la ujasusi la Marekani mjini Tehran

Kuhusu suala hilo, kila mara maafisa wa Iran wamekuwa wakiongezwa kwenye orodha hiyo kwa visingizio tofauti. Kwa kutekeleza vikwazo hivyo Marekani ilikuwa ikidhani kwamba ingeweza kuilazimisha Iran ipige magoti na kusalimu amri mbele yake lakini kinyume chake, nguvu ya Iran imekuwa ikiimarika siku baada ya nyingine katika nyanja mbalimbali na hata Marekani yenyewe imelazimika kuutambua rasmi mpango wa nyuklia wa Iran unaotekelezwa kwa malengo ya kiraia. Baada ya kutambuliwa rasmi mpango huo wa nyuklia wa Iran kupitia mazungumzo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), sasa Marekani imeamua kufanya nyama nyingine ya kuishinikiza Iran kwa kuzidisha vikwazo dhidi ya serikali ya Tehran ili kujaribu kudhoofisha nguvu yake ya makombora.

Mapatano ya JCPOA kati ya Iran na kundi la 5+1

Katika uwanja huo, Ross Letenin, mbunge wa Marekani alisema mwezi Machi uliopiata katika Kamati ya Uhusiano wa Kigeni ya Congress ya nchi hiyo kwamba shughuli za Iran zinazozua utata mkubwa zaidi baada ya kutiwa saini mapatano ya JCPOA ni mpango wa makombora wa Iran. Alisema ili kukabiliana na suala hilo Marekani itaiwekea Iran vikwazo vikali na vya kupoozesha ili isimamishe mpango wake huo.

Ni wazi kuwa Marekani haijapata funzo la kutosha kutokana na siasa zake mbovu za huko nyuma dhidi ya Iran na ingali inadhani kwamba itaweza kuilazimisha Iran isalimu amri kupitia vikwazo hivyo ambavyo huko nyuma vimeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa. Dakta Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema kuwa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran vinavunja moyo wa mapatano ya JCPOA na kuongeza kuwa vikwazo hivyo vitazidisha mivutano iliyopo kati ya nchi mbili hizi. Zarif alisema Jumanne katika mahojiano na televisheni ya CNN kwamba JCPOA ni mazungumzo ya pande kadhaa za kimataifa na hivyo hayawezi kuvunjwa na upande mmoja wala kujadiliwa upya na upande huo.