Marekani; muungaji mkono mkuu wa ugaidi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32040-marekani_muungaji_mkono_mkuu_wa_ugaidi_duniani
Kama inavyofanya miaka yote, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa ripoti kuhusiana na kile inachodai ni uungaji mkono wa baadhi ya nchi kwa ugaidi na kukabidhi ripoti hiyo kwa Congress ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2017 22:49 UTC

Kama inavyofanya miaka yote, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa ripoti kuhusiana na kile inachodai ni uungaji mkono wa baadhi ya nchi kwa ugaidi na kukabidhi ripoti hiyo kwa Congress ya nchi hiyo.

Katika ripoti hiyo, baadhi ya nchi zinazotuhumiwa kuunga mkono ugaidi zimeorodheshwa na marufuku pamoja na vikwazo vinavyotekelezwa dhidi ya nchi hizo kubainishwa. Kama ilivyotarajiwa nchi zinazokusoa na kupinga vikali siasa za kibabe za Marekani duniani ndizo zinazoongoza katika orodha hiyo. Katika Orodha hiyo Iran, Syria na Sudan zimetajwa kuwa waungaji mkono wakuu wa ugaidi kati ya nchi hizo zinazotuhumiwa na utawala wa Washington kuwa waungaji mkono wa ugaidi. Hii ni katika hali ambayo Marekani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi bali imekuwa na nafasi muhimu katika kuyabuni makundi hayo yanaoendelea kutekeleza jinai na mauaji katika pembe mbalimbali za dunia. Nyaraka na rekodi za serikali ya Marekani yenyewe zinathibitisha wazi kwamba kundi la kigaidi la al-Qaida lilibuniwa na shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA katika muongo wa 1980 kwa lengo la kupambana na Jeshi Jekundu la Shirikisho la Sovieti ya zamani nchini Afghanistan. Nusu karne baadaye, serikali hiyohiyo ya Marekani ilichukua hatua ya kuunda kundi jingine la kigaidi kama hilo kwa jila la Daesh kwa lengo la kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa ni kuenea ushawishi wa Iran na Ushia katika nchi za Asia Magharibi.

Daesh, moja ya makundi ya kigaidi na kitakfiri yaliyoundwa na Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani mwenyewe alimtaja mara nyingi Hillary Clinton Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa nchi hiyo katika serikali ya Barack Obama kuwa muhusika mkuu wa kubuniwa kwa kundi hilo la kigaidi katika Mashariki ya Kati. Michael Johns, mhariri wa gazeti la Vita vya Kiutamaduni anasema kuwa Marekani imebuni mipango kadhaa kuhusu eneo la Mashariki ya Kati na inafuatilia kwa karibu utekelezaji wake. Anasema kwa msingi huo, ripoti ya hivi karibuni ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kuhusiana na suala la ugaidi haina ukweli wowote kuhusiana na mambo yanayojiri katika eneo, bali imetolewa kwa msingi wa mitazamo maalum. Mhariri huyo anaendelea kusema kuwa Marekani inaendesha vita vya niaba katika eneo kwa kutegemea makundi hayo ya kigaidi ambayo anasema historia imethibitisha kwamba mwishowe huishia kuzikumba na kuzidhuru nchi zenyewe zilizoyabuni na kuyaunga mkono. Hii ni katika hali ambayo hatua ya kiongozi wa ngazi za juu zaidi kiutendaji nchini Mmarekani ya kutoa amri ya kuuawa watu wanaodhaniwa kuhusika na vitendo vya ugaidi tena bila ya kufikishwa mahakamani, ni mfano wa wazi wa ugaidi unaotekelezwa na nchi hiyo katika pembe tofauti za dunia. Mauaji hayo ambayo kimsingi hutekelezwa kwa ndege zisizo na rubani huwakumba wote, wadhaniwa wa vitendo vya ugaidi na vilevile wanawake na watoto wasio na hatia yoyote.

Trump akitiliana saini na Mfalme Salman wa Saudia mkataba wa mamia ya mabilioni ya dola

Wakati huohuo uungaji mkono wa Marekani kwa nchi zinazohusika moja kwa moja na ugaidi kama Saudia na utawala haramu wa Israel kwa hakika ni jambo linaloifanya Marekani kutofaa kabisa kuzituhumu nchi nyingine kuwa zinaunga mkono ugaidi. Marekani inasema kuwa ni dharura kukata misaada ya fedha na silaha kwa nchi zinazoshukiwa kushirikiana na makundi ya kigaidi katika hali ambayo yenyewe inatiliana saini na Saudi Arabia mikataba ya kijeshi inayogharimu mamia ya mabilioni ya dola; nchi ambayo jina lake liko kweye orodha ya faili la mashtaka ya familia za wahanga wa mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 mjini Washington na vilevile ni mdhamini mkubwa wa kifedha wa makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayotekeleza mauaji na jinai za kutisha katika pembe tofauti za dunia na hasa katika nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Marekani inashirikiana na Saudia kuwaua kigaidi watu wa Yemen

Kwa vyovyote vile ni wazi kuwa suala la mapambano dhidi ya ugaidi na kutolewa ripoti za kila mwaka za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu nchi zinazotuhumiwa kuunga mkono ugaidi si jingine bali ni mbinu inayotumiwa na nchi hiyo ya Magharibi kwa ajili ya kufikia malengo yake ya kidiploamsia kimataifa. La sivyo kama kweli Marekani ingetaka inasema ukweli kuhusiana na suala hilo ingekuwa ya kwanza kuliweka jina lake katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi duniani na kuamua kukata kabisa uhusiano wake na nchi kama Saudia. Hii ni katika hali ambayo kinyume na inavyodai, kila nchi au kundi linalopinga madai ya watawala wa Washington kuongoza dunia, huwekwa haraka tatika orodha nyeusi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya eti nchi zinazounga mkono ugaidi.