Kissinger: Kuwepo Daesh (ISIS) ni muhimu kwa ajili ya kuidhibiti Iran
Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger ameonya kuwa serikali ya Washington itafanya makosa kuliangamiza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) kwa sababu kuwepo kwake ni muhimu kwa ajili ya kuidhibiti Iran.
Kissinger, mwenye umri wa miaka 94 ambaye ni msomi mtajika anayetambulika kama mwanamkakati na mshauri muhimu kwa serikali ya Marekani, amesema endapo kundi la kigaidi la Daesh litaangamizwa katika Mashariki ya Kati, matokeo yake yatakuwa ni kuibuka kile alichodai kuwa ni 'Dola kuu lenye misimamo mikali la Iran' litakaloanzia Tehran na kusambaa hadi Beirut.
Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema ule msemo wa kale kwamba adui wa adui yako anaweza kuwa rafiki yako hauna matumizi tena hivi sasa kwa sababu Mashariki ya Kati ya sasa inauathiri ulimwengu kutokana na hali yake isiyotabirika ya mchemko na mchanganyiko wa idiolojia na harakati zake maalumu.
Amefafanua kuwa suala la kuliangamiza kundi la Daesh linaangaliwa kwa mtazamo mmoja na mataifa muhimu kadhaa ya Waislamu wa Kisuni na pia Iran ya Kishia na kuhoji, endapo maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi hilo yatabaki matupu ni upande upi utapaswa kuyadhibiti, muungano wa Kisuni au mrengo ulio chini ya udhibiti wa Iran?
Kissinger anatoa matamshi hayo katika hali ambayo, maeneo yaliyokuwa yamevamiwa na kukaliwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ni ardhi za mataifa ya Kiislamu ya Syri na Iraq.
Wataalamu wa siasa za Mashariki ya Kati wameyatafsiri matamshi ya waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwa ni ushahidi wa wazi wa kuthibitisha undumakuwili wa Washington katika vita dhidi ya ugaidi na kutilia nguvu hoja kwamba Marekani imekuwa ikiyasaidia na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kitakfiri likiwemo la Daesh ili kufanikisha malengo ya uwepo wake haramu katika eneo muhimu na hasasi la Mashariki ya Kati…/